MWILI wa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi,
leo utaagwa na viongozi wa kitaifa pamoja wananchi wa Jiji la Dar es
Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee, kabla ya kwenda kuzikwa katika Chuo
cha ugavi na ununuzi cha IPS kilichoko Chanika wilaya ya Ilala.
Msemaji wa familia, Edson Fungo aliliambia gazeti hili jana kuwa, kwa
kuwa Dk Masaburi alikuwa mwanasiasa na amewahi kushika nyadhifa
mbalimbali kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, familia
imeona vyema watoe fursa ya kuagwa na wanasiasa wenzake pamoja na wakazi
wa jiji la Dar es Salaam.
Dk Masaburi kabla ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, aliwahi kuwa
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Wakati akiwa Meya alichaguliwa pia
kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALART).
Hadi mauti yanamkuta, Dk Masaburi alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Magavana wa Chuo cha IPS kilichoko Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam.
Ni katika eneo la chuo hicho ndiko marehemu atazikwa leo. Ratiba
iliyotolewa na Msemaji huyo wa familia hiyo, inaonesha kuwa saa 3.00
mwili ndio utawasili kwenye Ukumbi wa Karimjee na ibada itaanza saa 4.00
asubuhi.
Utasomwa wasifu wa marehemu na baadaye kutakuwa na neno kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa serikali.
Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa 5.00 na saa 6.30
mchana msafara kwenda Chanika utaanza. Utakapowasili kutafanyika ibada
ya maziko na pia wananchi wa maeneo hayo na wanajumuiya ya IPS wataanza
kuaga.
Dk Masaburi aliaga dunia usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa
akisumbuliwa na homa ya Ini (Hepatitis B).
Habari ya kifamilia inaeleza Dk Masaburi alikuwa akisumbuliwa na homa
ya ini ambayo ilimsumbua kwa miezi kadhaa hadi mauti yanamkuta.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: