VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba leo wanashuka dimbani kusaka
pointi tatu muhimu ili kuzidi kujikita kileleni wakati watakapocheza
dhidi ya Kagera Sugar.
Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru huku Stand United wanaoshika
nafasi ya pili wakiwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa CCM
Kambarage, Shinyanga.
Hizi ndizo timu zinazokimbizana kwa pointi hivyo, macho yote
yataelekea kwao. Simba ndio vinara wa ligi kwa pointi 20 katika michezo
nane waliyocheza, wakijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja, tangu kuanza
kwa msimu huu.
Timu hiyo ya Msimbazi huenda ikaendeleza ushindi baada ya kutoka
kuifunga Mbeya City mabao 2-0 ugenini, kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini
Mbeya Jumatano.
Lakini pia, Kagera Sugar haiko katika kiwango kibaya msimu huu, kwani
inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 15 katika michezo tisa
iliyocheza.
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema anataka kuvuruga sherehe
za Simba kwa kuhakikisha wanainyamazisha. Licha ya tambo za wenyeji,
itakumbukwa msimu uliopita Simba ikiwa katika kiwango kibaya iliifunga
Kagera Sugar nyumbani na ugenini, ambapo kwenye Uwanja wa Taifa
ilishinda 3-1 na ugenini bao 1-0.
Mchezo huo huenda ukawa mgumu, kwani Simba itataka kushinda ili
kuendelea kubaki kileleni, na Kagera inataka ushindi iendelee kuwa
katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo yenye jumla ya timu 16.
Aidha, kama ilivyo kwa Simba hata Stand United imekuwa ni bora
ikijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja. Leo itaikaribisha African Lyon
kwenye Uwanja wa CCM, Kambarage Shinyanga. Timu hiyo msimu huu imekuja
kivingine baada ya kuwapiga vigogo wawili kwenye uwanja huo, yaani Yanga
na Azam zote zikifungwa bao 1-0 kila moja.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: