LEO ni Simba na Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zote
zikiwania ubingwa wa Ligi Kuu unaoshikiliwa na Yanga.
Azam inashika
nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 58
pointi saba nyuma ya vinara wa ligi Yanga yenye pointi 65 na ikiiacha
Simba inayocheza nayo leo kwa tofauti ya pointi moja.
Msimamo na hali halisi ya mbio za ubingwa unaashiria mchezo huo
utakuwa na ushindani wa hali ya juu, kwani kupoteza kwa timu moja ni
sawa na kujiondoa kwenye mbio za ubingwa msimu huu na pengine kutoa
nafasi kwa Yanga kutetea tena taji lake.
Timu hizo zinakutana zikiwa na historia tofauti ya mechi zao
zilizopita kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Majimaji ya
Songea na Simba kufungwa bao 1-0 na Toto Africans ya Mwanza kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kila timu itahitaji kushinda mechi ya leo kuweka hai matumaini yake
ya kutwaa ubingwa; Azam ikitaka kuendeleza wimbi la ushindi na zaidi
Simba ikiwania kusahihisha makosa yake kwa kuibuka na ushindi. Kwenye
mchezo uliopita timu hizo zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya mabao
2-2.
Azam wameonesha kuwa washindani wazuri kwa timu kubwa za Yanga na
Simba na hivyo mchezo wa leo unabeba taswira ya moja ya mechi kubwa
kwenye soka la Tanzania. Habari njema kwa Azam leo ni kurejea uwanjani
kwa mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Kipre Tchetche, ambaye
atashirikiana vyema na John Bocco.
Tchetche alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu
aliyopata kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika Uwanja
wa Manungu, Morogoro ambao Azam FC ilishinda bao 1-0. Simba yenyewe
katika ushambuliaji itategemea umahiri wa mfumania nyavu wake Hamis
Kiiza’Diego’ na mshambuliaji anayekuja vizuri Ibrahim Ajib.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: