Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema ana
wasiwasi Uwanja wa Karume, unaweza kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Hiyo inafuatia TRA kukamata magari matano ya TFF kutokana na deni la
kodi Sh. Bilioni 1 Milioni 118 ambazo ni malimbikizo tangu mwaka 2010,
wakati TFF ikiwa chini ya Rais Leodegar Tenga.
“Kwa kweli hali mbaya, na sitashangaa hata kesho Uwanja wa Karume nao
ukipigwa mnada, kwa sababu magari waliyokamata thamani yake haifiki
deni wanalodai,”amesema Malinzi.
Ofisa wa TRA, Richard Kayombo amesema wamekamata magari hayo ili kuwapa shinikizo TFF waweze kulipa madeni hayo.
Amesema deni hilo la Sh. Bilioni 1 na Milioni 118 ni malimbikizo ya
kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, zikiwemo za VAT na
mishahara ya wafanyakazi wake.
“Ikumbukwe awali tulikamata akaunti zao kwa sababu deni lilifikia
Bilioni 1. 6 na baada ya kupunguza deni tukawaachia akaunti zao, lakini
bado halijaisha na ndiyo sababu ya kukamata hayo magari matano,”amesema
Kayombo.
Ofisa huyo wa TRA amesema magari yote yaliyokamatwa, likiwemo basi la
wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars yapo kwenye kampuni minada ya
Yono.
Post A Comment: