WIKI moja baada ya Serikali kutangaza kuanzishwa kwa Divisheni ya
Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu, Rais John Magufuli
amewaibukia mawakili wa Serikali, akiwatuhumu kwa kushirikiana na
mawakili wa wahalifu ili Serikali ishindwe kesi. Aidha amewaonya polisi
kwa kuingia mikataba inayotia mashaka baina yao na wawekezaji.
Mahakama ya ufisadi inatarajiwa kutumika kushughulikia watuhumiwa wa
rushwa na ufisadi, wakiwemo waliokwisha tumbuliwa, lakini kesi zake
zinatarajiwa kuanza kunguruma Julai mwaka huu.
Akizungumza mkoani Dodoma jana wakati akifungua kikao kazi cha
makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali wa mikoa na
wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, Rais Magufuli alisema mawakili
hao wakiona kesi inayohusu fedha imeingia, wanasema ‘dili’ limeingia.
“Kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache,
nasema wachache... Panapokuwa na kesi inayohusu fedha, wana misemo yao
wanasema dili limepatikana.
“Saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wanashirikiana na mawakili
wa Serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu na wanaposhirikiana siku
zote Serikali inashindwa,” alisema.
Alionya kuwa hali hiyo inapoonekana kila siku Serikali inashindwa
katika kesi, kunakuwa na kigugumizi cha kuwezesha mawakili hao pale
wanapopeleka maombi. “Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na
upelelezi mtangulize maslahi ya nchi mbele,” alisema na kuongeza kuwa
amekuwa akisikitishwa na vitendo vya Serikali kushindwa katika kesi
nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: