MENEJA wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mkoani Pwani, Martin
Madulu, ametoa mwito kwa wananchi kufuata taratibu za kuunganishiwa
umeme, badala ya kujiunganishia kwa kuwatumia vishoka.
Mwito huo ulitolewa baada ya watu wanaotuhumiwa kujiunganishia umeme
bila kufuata utaratibu kukamatwa katika mtaa wa Kwamfipa wilayani hapa.
Alisema, kubainika kwa watu hao waliokuwa wanaiba umeme kumefuatia
taarifa za wancnchi kuhusu watu wanaohujumu miundombinu ya umeme katika
eneo hilo.
“Wezi hao walikuwa wamezichimbia nyaya za umeme chini ya barabara
kusambaza katika baadhi ya maeneo ikiwemo maduka, mabanda ya kuoneshea
video, hali ambao ni hatari kwa usalama wa watu na mali zao, pindi
majanga ya moto unaosababishwa na hitilafu ya umeme yanapotokea,”
alisema.
Ofisa Usalama wa shirika hilo, Henry Byarugaba alisema, Tanesco
inapata hasara kwa kupoteza mapato yake kutokana na wizi unaofanywa
kwenye miundombinu yake, pamoja na wasio waaminifu kujiunganishia umeme
kinyemela.
Byarugaba aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu
wanaojiunganishia umeme kinyume cha utaratibu ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yao.
Post A Comment: