SERIKALI ya China imekubali kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa reli ya kati ili kuharakisha utekelezaji huo ambapo imesema kuwa ipo tayari kuwashirikisha pia wadau wake wa masuala ya fedha na makampuni mbalimbali.
Balozi wa China hapa nchini Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing ametoa kauli
hiyo leo tarehe 25 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam alipokutana
na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli ambapo pia amemkabidhi barua yenye ujumbe kutoka kwa
Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping.
Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amemweleza Balozi Lu kuwa
Tanzania imedhamiria kuanza ujenzi wa Reli ya kati haraka iwezekanavyo
na tayari imetenga fedha kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika bajeti
yake ijayo kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
"Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya
uchumi katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na
kati zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio
maana hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze
na watu waanze kunufaika" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Balozi China hapa nchini Dkt. Lu Youqing amempongeza
Rais Magufuli na serikali yake kwa kujiandaa kwa fedha, vifaa na
rasilimali watu kwa ajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa na kwamba
Serikali ya China, Taasisi za fedha za China na Makampuni mbalimbali
yatatoa ushirikiano wote katika utekelezaji wa mradi huu.
"Kama ambavyo Prof. Mbarawa amefanya mazungumzo na Serikali ya China,
Taasisi za fedha za China na Makampuni, naahidi kuwa tutaanza kazi kama
ambavyo taratibu na viwango vya ujenzi vimewekwa, tutafanya kazi kwa
kujali muda, ubora na gharama nafuu" Amesema Balozi Lu.
Mradi mzima wa ujenzi wa reli ya kati unatarajiwa kugharimu Dola za
Marekani Bilioni 6.8 na umepangwa kutekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya
kwanza itahusisha ujenzi wa kilometa 1,216 za kutoka Dar es salaam -
Tabora - Isaka - Mwanza na itajengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na
China
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: