Serikali ya Kenya imewafuta kazi
maafisa wakuu wa Baraza la Mitihani Kenya (KNEC) kutokana na visa vya
udanganyifu vilivyoripotiwa wakati wa mitihani ya kitaifa mwaka jana.
Waliofutwa
kazi ni pamoja na afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo Bw Joseph Kivilu
na mwenyekiti wa bodi inayosimamia baraza hilo Bw Kibiru Kinyanjui.
Bw Kivilu pamoja na maafisa wengine saba wa baraza hilo wametakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi mara moja.
Tangazo
la kufutwa kwa wakuu hao limetolewa kwenye kikao cha wanahabari
kilichoandaliwa na Waziri wa usalama na masuala ya ndani Meja Jenerali
Joseph Nkaissery na Waziri wa Elimu Fred Matiang’i.
Bw Nkaissery amesema hatua zitachukuliwa dhidi ya waliohusika katika uadanganyifu huo.
Watahiniwa
waliopatikana na makosa ya udanganyifu mtihani wa kidato cha nne mwaka
2015 waliongezeka asilimia 70 kutoka mwaka uliotangulia.
Katika mtihani wa mwaka 2015, watahiniwa 5,101 waligunduliwa kuwa walitumia udanganyifu katika mtihani.
Mwaka
2014, ni watahiniwa 2,975 pekee waliokuwa wametumia hila katika mtihani
huo wakati huo visa vikiwa vimepungua kutoka visa 3,812 mwaka 2013.
Aliyekuwa naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Prof George Magoha
ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo na ataanza kufanya kazi
mara moja.
Muda mfupi baada ya tangazo la kufutwa kwa wakuu hao
kutolewa, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakieleza hisia
zao na kitambulisha mada #KNEC kimeanza kuvuma.
Post A Comment: