TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo inashuka Uwanja
wa Ommisports Idriss Mahamat Ouya jijini ND’jamena kuwavaa wenyeji Chad
katika mchezo wa kuwania fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kikosi cha Stars kikiongozwa na Kocha Mkuu Charles Mkwasa kiliwasili
nchini humo kwa ajili ya mchezo huo muhimu kuhakikisha wanapata ushindi
wa ugenini kabla ya kurudiana Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka
Kizuguto ilimkariri Mkwasa akisema wamejipanga vizuri na wanatarajia
kung’ara leo.
“Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo huu wa
ugenini ili tutakaporudi nyumbani tutumie pia vyema uwanja wetu, ”
alisema Mkwasa.
Licha ya kukabiliwa na mchezo huo muhimu, kikosi cha Taifa Stars
kiliwasili kwa mafungu kutokana na wachezaji wengi kukabiliwa na
majukumu katika timu zao, ambapo zilikuwa kwenye michezo ya Ligi ya
Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho mwishoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa Kizuguto, kikosi cha Taifa Stars kimekamilika baada ya
kuwasili kwa nahodha wa timu hiyo anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji,
Mbwana Samatta na mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taifa Stars inakutana na Chad ambayo si miongoni mwa nchi
zinazojulikana katika soka, ikiwa inashika nafasi ya 127 katika ubora wa
viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), huku Tanzania ikiwa
ni ya 125.
Hadi sasa Taifa Stars inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo la G
ikiwa imecheza mechi mbili ikiwa na pointi moja, ambapo ya kwanza
ilifungwa mabao 3-0 na Misri mjini Cairo, kisha ikatoka 0-0 na Nigeria
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Misri inaongoza Kundi G ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi
zote mbili ikiifunga Taifa Stars na Chad, wakati Nigeria inashika nafasi
ya pili baada ya kuifunga Chad na kutoka sare na Taifa Stars, huku Chad
yenyewe ikiburuza mkia baada ya kupoteza mechi zote mbili ilizocheza.
Kwa mazingira hayo ni wazi Taifa Stars ina kila sababu ya kushinda
leo na kujiweka katika nafasi nzuri katika michezo ya marudiano kwa
kundi hilo.
Post A Comment: