Mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam, Abraham Warioba (50), amehukumiwa
kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh milioni 39, baada ya
kupatikana na hatia ya kumiliki digidigi 20 kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya
Ilala, Juma Hassan, baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi
uliowasilishwa mahakamani hapo na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka
ambao ni Jamhuri.
Hata hivyo, Warioba ambaye ni mfanyabiashara hakuwapo mahakamani
baada ya kuruka dhamana wakati shahidi wa tatu akiwasilisha ushahidi
wake, hivyo ataanza kutumikia adhabu hiyo pindi atakapotiwa mbaroni.
“Mahakama inamtia hatiani mtuhumiwa kwa kumiliki digidigi 20 ambao ni
nyara za Serikali, huku akiendelea kutumia vibali vilivyokwisha muda
wake jambo ambalo ni kinyume cha sheria, hivyo atatumikia kifungo cha
miaka 20 gerezani au kulipa faini shilingi milioni 39, adhabu hii
itaanza mara tu baada ya kukamatwa.
“Kwani alipo ni rahisi tu kuweza kukamatwa kwa kuwa kila kitu kipo
cha kumfanya akamatwe, hivyo mahakama inatoa amri akamatwe ili iwe
fundisho kwa wote wenye tabia za kumiliki nyara za Serikali kinyume cha
sheria,” alisema Hakimu Hassan.
Kesi hiyo ilikuwa na mawakili wawili wa Serikali ambao ni Florida
Wenceslaus na Chesense Gavyole, ambao waliiambia mahakama hiyo kuwa
hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo
kuiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote wenye
tabia kama hiyo ya kumiliki nyara za Serikali bila kuwa na vibali
halali.
Katika hati ya mashtaka, Warioba anadaiwa Januari 17 mwaka 2011 eneo
la Pugu Kigogo Fresh, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alikutwa
akimiliki digidigi 20 wenye thamani ya Sh. milioni 3.9 ambao ni nyara za
Serikali, huku vibali vyake vya kumiliki wanyama hao vikiwa vimeisha
muda wake jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Post A Comment: