Zikiwa
zimepita siku tano tangu Rais John Magufuli aeleze kushangazwa na
vitendo vya askari wa polisi kunyang’anywa bunduki na majambazi, polisi
mkoa wa Dodoma wameporwa SMG.
Watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi walifanya uporaji huo baada
ya kuvamia ofisi za kampuni ya simu za mikononi ya Halotel katika eneo
la Medelii, Manispaa ya Dodoma, na kuwajeruhi askari polisi waliokuwa
zamu.
“Ni aibu kumuona askari Polisi mwenye silaha ananyang’anywa silaha,
ni aibu, na nasema hiyo ni aibu... mpaka jambazi akunyang’anye silaha
na wewe una silaha?” Alihoji Rais Magufuli.
Rais Magufuli alizungumzia udhaifu huo siku tano zilizopita
alipokuwa akihakiki bunduki zake mbili, shortgun na bastola, ikiwa ni
utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa
wakazi wote.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa hapa, David Mnyambuga,
tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana, saa nane na nusu usiku
katika ofisi hizo.
Alisema watu hao wakiwa na mapanga na nondo, walivamia ofisi hizo
na kutoboa ukuta na kisha kuwajeruhi askari polisi kwa mapanga na kupora
SMG hiyo.
Aidha, alisema katika tukio hilo baadhi ya askari walipatwa na
majeraha madogo ambapo walitibiwa na kuruhusiwa lakini Shadrack
aliyejeruhiwa kichwani alilazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla
ya kuruhusiwa jana asubuhi baada ya afya yake kuimarika.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa alisema jeshi hilo linamshikilia mtu
mmoja ambaye anaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo, na kwamba
msako mkali bado unafanyika ili wahusika wote waweze kukamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
CHANZO:
NIPASHE
Post A Comment: