Mabalozi kutoka Marekani na Nchi za Umoja wa Ulaya, wameendelea
kuonyesha msimamo wao wa kutoridhishwa na uchaguzi wa marudio Zanzibar
baada ya jana kususia mwaliko wa kushiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais
wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wanadiplomaasia hao walipewa mwaliko rasmi na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ), lakini waliiambia kuwa hawatashiriki sherehe hizo.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Silima Kombo Haji, amesema kuwa serikali ilitoa mwaliko rasmi kwa Mabalozi wote wa nchi za
Afrika na Ulaya kuhudhuria sherehe hizo, lakini Mabalozi wa Umoja wa
Ulaya na Marekani walijibu kuwa hawatahudhuria bila kutoa sababu zozote.
“Tumewaalika na mialiko imewafikia na kutujibu kuwa hawatahudhuria. Hatukuwa na sababu ya kuwang’ang’ania," alisema Haji.
Hata hivyo, alisema licha ya Mabalozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya
kutohudhuria sherehe hizo, Mabalozi wa nchi nyingine walioalikwa
walihudhuria sherehe hizo na wengine kutuma wawakilishi wao.
Aliwataja Mabalozi wa nchi waliohudhuria sherehe hizo ambao wengi
ni kutoka nchi za Afrika kuwa ni Balozi wa Cuba, Zimbabwe, DRC,
Indonesia, Iran, Kenya, Kuwait, Malawi, Msumbiji na Oman.
Wengine ni Palestina, Ruwanda, Algeria, Angola, Burundi, China,
Japan, Libia, Pakistan, Umoja wa Nchi za Kiarabu, India, Uganda,
Uturuki, Urusi na Mratibu Mkaazi wa UN.
Post A Comment: