Mshambuliaji wa FC Barcelona, Luis Suarez amerejea kwa mara ya kwanza
kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uruguay kwa ajili ya mchezo wa
kimashindano, baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo tisa na
shirikisho la soka duniani FIFA.
Suarez, alitajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa lake, kwa ajili ya
mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka
2018, na tayari amejiunga na wenzake kambini mjini Montevideo nchini
Uruguay.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, aliruhusiwa kucheza
michezo ya kimataifa ya kirafiki baada ya kushinda rufaa yake ya
kufungiwa kwa kipindi cha miezi minane pamoja na kucheza soka kwa
michezo tisa, kufuatia kosa la kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia
Giorgio Chiellini, wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014.
Akiwa katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Brazil
utakaochezwa mwishoni mwa juma hili, Suarez ameonekana ni mwenye furaha
na wakati wote alionyesha ushirikiano wa kutosha kwa wachezaji wenzake.
Hata hivyo alipata nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari akiwa
katika kambi ya timu ya taifa, na kuonyesha kujutia kosa alilolifanya
wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 kwa kung’ata mchezaji
wa Italia pamoja na kuushika mpira kwa makusudi wakati wa fainali za
kombe la dunia za mwaka 2010 zilizochezwa nchini Afrika kusini.
Post A Comment: