Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Jackson Mayanja ameonyesha kuridhia
hatua ya kurejea kwa beki Hassan Isihaka, ambaye alikua kifungoni
kutokana na utovu wa nidhamu aliouoyesha mwezi uliopita.
Mayanja, amesema mchezaji huyo sasa anaonekana kuwa amejifunza kwa
kipindi chote alipokuwa nje ya timu na hali hiyo ndiyo anayoitaka iwepo
kwa wachezaji wote ndani ya kikosi chake kwa kumuheshimu kocha.
Kocha huyo aliyejiunga na klabu ya Simba akitokea kwenye klabu ya
Coastal Union ya jijini Tanga, ameongeza kwa kusema kuwa mchezaji
anapokuwa na nidhamu ni rahisi kukaa na kocha kwa muda mrefu na
kujitengenezea mazingira ya kupangwa katika kila mchezo kwa kuwa atakuwa
akiyapokea vizuri maelekezo.
“Isihaka amerejea akiwa amebadilika na anaendelea na wenzake kama
kawaida, lakini nikwambie kwamba mchezaji yeyote mwenye nidhamu kwa
kocha wake ujue atakuwa na mafanikio makubwa hata kwa siku za usoni,
lakini kama atakwenda kinyume na hapo unadhani mwalimu gani
atakayethubutu kumsajili kama akijua nidhamu yake ni mbovu? Alihoji
Mayanja.
Kuhusu kukosekana kwa mlinzi mwingine Abdi Banda anayesubiri maamuzi
ya kamati ya nidhamu ya Simba, kufuatia kitendo cha utovu wa nidhamu
aliouonyesha wakati wa mchezo wa dhidi ya Coastal Union huko jijini
Tanga, Mayanja amesema kukosekana kwake hakutampa wakati mgumu kwani
wapo wachezaji wenye uwezo mkubwa kuliko yeye.
Amesema hata hivyo Banda hakucheza michezo mingi iliyopita, hivyo
hakumsumbui hata kidogo, huku akirejea suala la kumtumia mchezaji
kutokana na nidhamu yake ndani na nje ya uwanja.
Post A Comment: