HUKU zikiwa zimebakia mechi sita kabla ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, vinara wa ligi hiyo, Simba, wanaonekana kuwa na mchezo mmoja mgumu, mingine mitano ikiwa mteremko, huku mahasimu wao Yanga wao wakitakiwa kukaza buti kutokana na kukutana na timu ngumu.


Katika michezo hiyo sita kwa timu hizo za Simba na Yanga, kila moja itakuwa na michezo mitatu uwanja wa nyumbani na mitatu ugenini, ambapo timu itakayofanya vizuri kwenye michezo hiyo itajitengenezea mazingira mazuri ya kuusogelea ubingwa.

Michezo hiyo sita kwa upande wa Simba ni dhidi ya Tanzania Prisons, Lipuli FC, Ndanda FC, Singida United, Kagera Sugar pamoja na Majimaji, ambapo katika michezo hiyo wenyewe wanaouhofia zaidi ni ule dhidi ya maafande hao wa Prisons utakaochezwa Novemba 19, mwaka huu, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Huo ndio mchezo unaowaumiza zaidi vichwa, kwani Prisons ni moja ya timu ngumu hasa wanapokuwa uwanja wao wa nyumbani, huku mchezo dhidi ya Singida United ambayo ni tishio kutokana na usajili wao mzuri, wakiuona hauna madhara sana kwani utachezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Michezo dhidi ya Ndanda FC na ule dhidi ya Kagera Sugar, pia haiwatishi sana licha ya kwamba watachezea ugenini, kwani timu hizo zinaonekana kulegalega msimu huu, huku wakiwa na uhakika wa kuwaangamiza Lipuli FC na Majimaji katika michezo ambayo itachezwa Uwanja wa Uhuru.

Kwa upande wao Yanga wanaonekana kuwa na michezo migumu minne, huku miwili wakionekana kuwa na uhakika wa kushinda ambayo ni dhidi ya Mwadui FC na ule dhidi ya Ruvu Shooting; yote ikichezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Michezo ambayo inawaumiza vichwa Wanajangwani hao ni ule dhidi ya Mbeya City na Prisons ambazo licha ya kwamba watakuwa Uwanja wa Uhuru, lakini timu hizo hazitabiriki huku pia wakiwaza namna ya kuwakabili Mbao FC, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kazi kubwa ikiwa tena Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Azam, mchezo wa funga dimba mzunguko huo wa kwanza.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: