ads

MAMBO mapya yameibuka kumhusu, Dk. Louis Shika, ambaye hivi karibuni aliibuka mshindi wa mnada wa nyumba za kifahari za mfanyabiashara Said Lugumi zilizoko Mbweni JKT na Upanga jijini Dar es Salaam lakini akashindwa kutimiza masharti ya mnada hivyo kujikuta akiwa mikononi mwa dola.


Miongoni mwa mambo hayo ni makazi yake jijini Dar es Salaam pamoja na uhalali wa udaktari wake licha ya kwamba aliwahi kukaririwa kuwa ni msomi wa shahada ya uzamivu (Ph.D).

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambalo linaendelea kumhoji pamoja na kufanya upekuzi nyumbani kwake Tabata Mawenzi, limesema hata udaktari wake unatia shaka kwa kuwa ameshindwa kuonyesha vielelezo kuthibitisha anastahili hadhi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alisema wanaendelea na upelelezi dhidi ya mtu huyo na jana walikwenda kumkagua nyumbani kwake Tabata Mawenzi.

Pia alisema Shika hana taalamu ya udakatri na kwamba inasemekana huenda alitumwa na Lugumi mwenyewe kuharibu mnada huo baada ya kushindwa kutoa fedha ambazo alidai ziko nje ya nchi.

“Tulipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Yono Auction Mart, Stanley Kevela, kuwa huko Mbweni JKT wakiwa wanafanya mnada wa hadhara wa kuuza nyumba za mfanyabiashara Lugumi, alijitokeza mtu anayeitwa Shika  ambaye alishinda mnada huo kwa kutaka kununua nyumba zote tatu, kumbe hakuwa na fedha,” alisema Mambosasa.

Mambosasa alisema ‘tajiri’ huyo alitaka kununua nyumba moja ya Mbweni kwa Sh. bilioni 1.2, nyumba ya pili iliyoko pia Mbweni Sh. milioni 900 na nyumba ya tatu iliyoko Upanga  alishinda na kutaka kununua kwa Sh. bilioni 1.2.

“Mtuhumiwa huyo alitakiwa kulipa asilimia 25 ya fedha kwa kila nyumba lakini hakuwa na fedha ndipo walipomkamata na kumfikisha kituo cha polisi kwa hatua zaidi. Upelelezi unaendelea na atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,” alisema.

Aidha, Kamanda Mambosasa alisema taarifa zinaonyesha kuwa inawezekana alitumiwa na Lugumi mwenyewe kwa kuwa alivyotakiwa kutoa fedha alisema ziko nchini Russia na Lugumi hajulikani mahali anapoishi kwa sasa.

“Tunaendelea kumhoji na leo (jana). Askari walienda kumkagua nyumbani kwake,” alisema Kamanda Mambosasa
Pia alisema wanaendelea kumhoji na kwamba hadi wakati huo taaluma ya udaktari aliyoitaja alikuwa hajaithibitisha kwa kutoa vielelezo.

“Amesema ni daktari lakini hajathibitisha kwa hiyo udaktari wake hadi sasa ni wa madai, hivyo amefanya kazi wapi hajatuambia. Sifahamu ila amesema ni mkazi wa Tabata Mawenzi,” alisema.

Alipohojiwa na waandishi wa habari juzi jioni, Shika alisema yeye ni Rais wa kampuni ya kimataifa inayoitwa Ralcefort yenye Makao Makuu yake nchini Russia na kwamba wanaingia Tanzania kwa lengo la kutekeleza sera ya Rais John Magufuli ya uchumi wa viwanda.

Alisema kampuni hiyo inashughulika na utengenezaji wa kemikali ingawa watakapokuja Tanzania watabadilisha kulingana na mahitaji ya nchi.

“Unapohamia mahala unahitaji sehemu ya kukaa. Tunapoingia Afrika tunahitaji mahali pa kukaa wafanyakazi wetu, hivyo naamini Watanzania watashirikiana na wafanyakazi wetu ili tujenge nchi vizuri,” alisema Shika.

Aidha, alisema wanatarajia kujenga viwanda 30 Tanzania ambavyo vitazalisha aina mbalimbali za bidhaa zikiwamo za vyakula na petroli.

Umaarufu kwenye mitandao ya Kijamii

Dk. Luis Shika amepata umaarufu wa chee na sasa amegeuka kuwa mjadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Tangu ashinde kununua nyumba hizo ilihali hana hata senti mfukoni, Dk. Shika amekuwa akitajwa sana kwenye mitandao mingi ya kijamii kuliko mtu mwingine.

Katika mitandao ya WhatsApp, Facebook na Instagram, watu wamekuwa wakituma ujumbe mbalimbali wa kufurahisha kuhusu ‘tajiri’ huyo.

Ujumbe mmoja uliotumwa kwenye WhastApp na kusambaa kwenye makundi mengi ni ule wenye picha yake unaosema “jamani bilionea Dk. Luis anawatakia usiku mwema.”

Picha nyingine maarufu ambayo imesambaa kwenye makundi ya WhastApp ni ile inayomwonyesha akiwa pembeni ya bilionea namba mbili duniani, Bill Gate, iliyosema “mabilionea duniani huvaa simple”.

Ujumbe mwingine ambao umekuwa ukisambaa kwenye makundi hayo ni ule unaosema: “ reaking News Dr. Luis Shika ametangaza kuinunua Klabu ya Simba atakapotoka Central”.

Mmoja wa wachangiaji kwenye kundi moja la WhatsApp alisema mnunuzi huyo wa majumba ya Lugumi ni noma maana
alipomuuliza kwani anafanya kazi wapi alianza kwa kumzodoa.

“Yule jamaa kweli noma, mimi nilikuwapo kwenye mnada na nilifanya naye mahojiano nikamuuliza mzee unafanya kazi gani akaniambia mimi siyo mzee ni Doctor with Ph.D na ni mtaalamu wa kemikali na ni Rais wa Kampuni ambayo Makao Makuu yake yako Moscow, Russia,” alisema.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: