
MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), ameitahadharisha serikali kuhusu mpango wake wa kuwekeza kwenye miradi mikubwa kwa kutumia fedha za mikopo kuwa unaweza kuua uchumi wa taifa.
Waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika serikali ya awamu ya tano, pia ameitaka serikali kuruhusu sekta binafsi kuwekeza katika miradi mikubwa badala ya serikali kutumia fedha zake kuitekeleza.
Aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana alipochangia mjadala kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019.
Nape alisema katika mpango huo umeainisha miradi aliyoiita ya aina mbili -- ya huduma za kijamii na ya kibiashara. Alisema miradi ya huduma za jamii kama vile maji, afya, elimu na utawala bora kwa asili yake haiendeshwi kibiashara.
“Sehemu ya pili kuna miradi ambayo kwa asili yake inaweza kuwekezwa kibiashara. Miradi hii ni ya uzalishaji wa umeme Stigler’s George, ujenzi wa reli, uboreshaji wa shirika la ndege, bandari na barabara ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara na ikajilipa. Sababu za kuchukua hela za serikali na kupeleka huko kwa kweli sijaiona," alisema.
"Nimeshtuka kidogo kuona serikali inapendekeza kuwekeza fedha za serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi kwa kutengeneza mazingira kwa sekta hiyo kuwekeza kwenye miradi hii badala ya kuchukua fedha za serikali na kupeleka kule kwani madhara yake ni makubwa na mpango huu ukitekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.
Nape alisema miradi hiyo ina gharama kubwa ya mabilioni ya Dola za Marekani na uwekezaji wake utachukua muda mrefu, hivyo muda wa faida yake (payback period) kuwa mrefu.
Aliongeza kuwa tafsiri ya uamuzi wa kutumia fedha za serikali kwenye miradi hiyo ni kwanza, itailazimisha serikali kutumia fedha nyingi hivyo lazima iende kukopa, na ikikopa itaanza kulipa deni lililokopwa kabla ya miradi kuanza kulipa faida kwa nchi.
"Kwa hiyo, tutachukua hela kwenye maeneo mengine tulipie deni kwenye miradi hii na kufunga mikanda muda mrefu," Nape alisema na kuongeza:
"Kwa nini serikali inafikiri kwamba kuwekeza pesa za serikali kwenye miradi ambayo ingeweza kuwekeza kibiashara na sekta binafsi ni jambo la tija kwa nchi yetu? Nadhani hapana.”
"Ukichukua pesa za maeneo mengine maana yake utaathiri miradi ya huduma, elimu, afya na itafika mahali hata fedha za wafanyakazi itashindikana kulipwa. Kuna madhara makubwa kwa Deni la Taifa kuchukua hela za serikali ambazo ni lazima kukopa kuwekeza kwenye miradi hii.
"Hapa ndiyo ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu kuishauri serikali na Rais kuwekeza hela za serikali kwenye miradi hii, napata tabu sana."
Alisema kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa bungeni mjini hapa Jumanne na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Deni la Taifa limefikia Dola bilioni 26, ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wake na ukomo ni asilimia 56.
"Kwa mfano, miradi hii mitatu ukiacha hiyo miradi mingine ya huduma za jamii; mradi wa kwanza wa ujenzi wa reli ya kati (Standard Gauge) tathmini yake unaweza kugharimu Dola bilioni 15, mradi wa uzalishaji umeme unaweza kugharimu Dola bilioni tano na uboreshaji wa Shirika la Ndege (ATCL) utagharimu Dola bilioni moja, jumla itakuwa Dola bilioni 21, hivyo ukiwa na dola bilioni 26, Deni la Taifa, ukijumlisha na Dola billion 21 itakuwa Dola bilioni 47. Maana yake hii 'imebust' na tunakwenda kutokopesheka," Alisema.
Alishauri serikali kuachana na alichokiita fikra ya kuandika kwenye makaratasi kuwa inatumia sekta binafsi ilhali haitumii badala yake ianze sasa kuitumia sekta hiyo kwa vitendo.
Alisema awamu ya pili ya serikali chini ya Mzee (Ali Hassan) Mwinyi iliruhusu sekta binafsi, ya tatu na ya nne ambayo Rais wa sasa alikuwa Waziri wa Ujenzi wakati wake waliruhusu makandarasi kutoka sekta binafsi wakachukua mikopo ya benki wakaanzisha kampuni lakini leo watu hao 'mortgage' zao zinauzwa kwa sababu wana madeni.
Alisema watu hao wanaidai serikali wakati serikali imeanza kuchukua mkondo wa shughuli zake za ujenzi kuchukuliwa na serikali yenyewe, hivyo hawa muda wote wanakufa kikazi.
Naye Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), alisema anashangaa kuelezwa na serikali kwamba uchumi wa Tanzania unakua, lakini kwa kuangalia vigezo vya uchumi kukua, anaona hali halisi ya Mtanzania inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliitaka serikali kueleza kuna mikakati gani ya kufanya mapinduzi ya kilimo akiamini kuwa kutowekeza katika sekta hiyo kutaifanya serikali kuendelea kusema maneno wakati hakuna kitu kinachofanyika.
Mbunge wa Maelezo, Saada Mkuya, Salum (CCM), alisema kuna haja serikali kutoipa kisogo Zanzibar katika utekekezaji wa azma yake ya kuwa na Tanzania ya viwanda.
"Kwenye eneo la utalii na masoko kwa namna yoyote unapotaka kutangaza utalii huwezi kuacha Zanzibar, lakini mpango huu hakuna kitu hicho na anaweza kusema si jambo la muungano. Sasa kwanini wabunge wa muungano tupo 53 humu?" alihoji.
Jaku Hashim Ayoub, Mbunge anayewakilisha Baraza la Wawakilishi (CCM), alimshauri Dk. Mpango kukaa na wafanyabiashara ili kuwasikiliza na kutatua kero zao kwa lengo la kuinua biashara na kuongeza mapato ya nchi.
Mbunge wa Kiteto, Emmanuel John (CCM), alisema ipo haja serikali kuangali upya sekta ya kilimo ili mazao kama mahindi nayo yatangazwe kuwa ya kibiashara.
"Zao la mahindi liwe la biashara sasa. Mtu alime halafu aruhusiwe kupeleka mazao yake anakotaka kwenda kuuza. Suala hili liingizwe kwenye mpango," alisema huku akiikumbusha pia serikali kuwekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu baharini.
Post A Comment: