ads

IKIWA imebaki siku moja kabla ya kumalizika kwa muda aliotoa Rais John Magufuli kwa wamiliki wa vituo vya mafuta kufunga mashine za kielektroniki (EFD) vinginevyo wafutiwe leseni, vingi vimeonekana kutii agizo hilo.


Julai 19 Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Biashara na Uwekezaji kuhakikisha ndani ya siku 14 wamiliki wa vituo vya mafuta wawe wamefunga mashine za EFD ili kudhibiti mapato ya serikali.

Katika agizo hilo, Rais Magufuli aliagiza mmiliki yeyote atakayekiuka agizo hilo afungiwe ikiwamo kufutiwa leseni yake ya biashara.

Jana gazeti la  Nipashe lilizunguka katika baadhi ya vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam na kushuhudia vikiwa vimefunga mashine hizo huku vikiwa vinatoa risiti kwa wateja waliokuwa wanahudumiwa.

Baadhi ya vituo ambavyo gazeti hili lilitembelea ni pamoja na kituo cha Oil Com cha Mbuyuni Kunduchi, Oil Com Afrikana, Total ya Makonde, vyote wilayani Kinondoni na Oil Com Barabara ya Nyerere, Oil Com Barabara ya Nyerere na DBP cha Nkurumah wilayani Ilala.

Vingine ni Total ya Morocco, Oryx Victoria, Oil Com Victoria, Big Bon ya Sinza, Lake Oil Sinza, TSN Bamaga, Total Mliman City, Puma Mwenge na Total Mbuyuni, Osterbay, vyote wilayani Kinondoni.

Baadhi ya wauzaji katika vituo hivyo hawakutaka kuzungumzia mwamko wa matumizi ya mashine baada ya tishio la kufutiwa leseni kwa madai kuwa si wamiliki.

“Unajua unaponihoji suala la kufunga mashine, unakuwa haunitendei haki kwa sababu mimi ni mfanyakazi tu, bosi wangu ndiye anaamua kufunga ama kutokufunga," alisema muuza mafuta mmoja katika kituo cha Oil Com Mbuyuni.

"Kazi yangu ni kufanya kazi tu, kwa hiyo labda angekuwapo yeye ndiye angefaa kulizungumzia.”

Mapema mwezi uliopita TRA ilifungia vituo vya mafuta kote nchini ambavyo havikuwa vikitumia mashine hizo baada ya kupokea agizo kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo baada ya kushuhudia mapungufu akiwa katika ziara ya kushtukiza jijini Dar es Salaam ambako yeye mwenyewe alifungia vituo vya Oli Com Kigamboni na GBP Uwanja wa Ndege.

Akiwa ziarani Biharamlo, Rais Magufuli ‘alipigilia msumari’ suala hilo kwa kurudia tena kuwataka wenye vituo kuhakikisha wanafunga mashine hizo ndani ya muda aliowapa.

Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ben Mwaipaja, alisema agizo la Rais Magufuli limetekelezwa kwa asilimia kubwa mpaka sasa.
Alisema tangu kutolewa kwa agizo hilo, wamiliki walijitokeza kwa wingi kuagiza mashine hizo na kwamba wanaamini hadi kesho watakuwa wamefunga wote.

“Tunashukuru sana wamiliki wa vituo hivi, kwa kweli wameitikia agizo la Rais, wengi wamefunga na hivi tunavyozungumza kuna mashine nyingine zinaendelea kusambazwa kwao,” alisema Mwaipaja. "Tunawapongeza kwa hilo."
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: