ads

MARAIS John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda, wameweka historia barani Afrika, baada ya kuzindua mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Chongoleani, Tanga hadi Hoima nchini Uganda, ambalo litakuwa refu kuliko yote duniani baada ya kukamilika.


Bomba hilo litakalogharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 (sawa na Sh. trilioni nane), linatajwa kuwa litakuwa la kwanza kwa urefu duniani katika usafirishaji mafuta ghafi kwani urefu wake utakuwa kilomita 1,445. Kwa sasa bomba refu kuliko yote duniani ni lile lililoko India lenye urefu wa kilomita 600, kwa mujibu wa Rais Magufuli.

Ujenzi wa bomba hilo unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 lakini Rais Magufuli aliwataka makandarasi wanaofanya kazi hiyo kuharakisha ili limalizike mapema kwa nia ya kuchochea ukuaji wa uchumi kwa Tanzania na Uganda.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi kuzindua mradi huo, hafla iliyoshuhudiwa na viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka Tanzania na Uganda, alisema makandarasi hao wana uwezo mkubwa hivyo wafanye hima kumaliza ujenzi mapema ili kuwanufaisha wananchi.

Alisema bomba hilo litanufaisha nchi husika pamoja na Afrika Mashariki kwa ujumla na kwamba litapita kwenye wilaya 24, mikoa minane na vijiji 180.

Hata hivyo, alisema wananchi wote ambao watapitiwa na mradi huo katika maeneo hayo watalipwa fidia, isipokuwa wale ambao wanaanza kujenga nyumba baada ya tathmini kufanyika.

“Mradi huu utumike kwa maendeleo ya nchi zetu. Nafahamu tumeanza kulipa fidia, huku wengine wakianza kujipanga eneo linakopita bomba kwa kujenga nyumba wakiamini watalipwa fidia. Lakini niwaambie watakaolipwa ni wale walipigwa picha wakati ule, ukijenga sasa hivi utakuwa umeula wa chuya,” alisema.

Alieleza kuwa baada ya mradi huo kukamilika wataalamu waliotumika kugundua mafuta, pia watatumika kugundua mafuta yanayokisiwa kuwa kwa kiwango kikubwa cha Ziwa Tanganyika na Eyasi, ili kuyachimba na kujenga bomba kuunganisha na bomba hilo.

Rais pia alisema bomba hilo si la kwanza nchini kwa kuwa Tanzania ina uzoefu katika ujenzi wa mabomba kama hayo, kwa kuwa tayari kuna bomba la gesi la Songosongo hadi Dar es Salaam lenye kilomita 232, Mnazi Bay hadi Dar es Salaam  522 na bomba la Tazama linalotoka Kigamboni hadi Ndola, Zambia lenye kilomita 1,710.

Alisema serikali itajenga pia bomba litakalosafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Tanga, ambako litajengwa bomba lingine la gesi hadi Uganda kwa ajili ya kuyeyusha chuma.

MUSEVENI ALONGA
Awali, Rais Museveni aliishukuru Tanzania kwa kuikubalia Uganda kujenga bomba hilo ambalo litasaidia kushusha bei ya mafuta nchini mwake. Pia alisema Tanzania imetoa somo kwa Uganda kwa kufufua shirika la ndege (ATCL).

“Kama Tanzania ilivyofanya kufufua ndege zake, Uganda pia hivi karibuni tutazifufua na zitapata nafuu ya mafuta yatakayopita kwenye bomba hili na pia mafuta kupata, petroli, dizeli, mafuta ya ndege. Mafuta pia yatatusaidia katika kuzalisha umeme na hata kuboresha kilimo kuwa cha kisasa,” alisema.

Alisema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatumia Dola za Kimarekani bilioni 1.6 kila mwaka kwa kuagiza bidhaa za chuma nje, ambazo hutumika katika ujenzi wa majengo, madaraja, reli na matumizi mengine.

“Sasa nchi za EAC zitaimarisha uchumi wao na kwamba ujenzi wa bomba hili utakuwa hauna gharama ya usafirishaji, VAT (kodi ya ongezeko la thamani), hakuna ‘corporate income tax’ (kodi ya mapato ya kampuni). Ingawa bei ya mafuta imeshuka duniani kutoka
Dola za Kimarekani 120 kwa pipa na kufikia dola 50, kwa mradi huu serikali ya Tanzania imetupunguzia gharama na kodi ambayo ingepandisha bei ya mafuta,” alisema.

Alisema mradi huu utazinufaisha nchi hizo hususan katika biashara ndogo ndogo za wajasiriamali na usambazaji wa vifaa vya ujenzi kama vile saruji.

“Tunahitaji kuibadili jamii yetu kiuchumi, tutumie rasilimali zetu katika kujenga barabara, maeneo ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo bora na reli bila kutegemea mikopo. Sasa ni wakati wa kusonga mbele na hakuna wa kutusimamisha,” alisema Rais Museveni.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: