KIPA mpya wa Simba, Aishi Manula ameweka bayana kuwa, atahakikisha anaifanya kazi yake vizuri ipasavyo kwa lengo la kuiwezesha timu hiyo kufikia malengo yake, huku akiwaambia Wanasimba kwamba wasiwe na wasiwasi, wajiandae kufurahi tu.
Manula ambaye ametua Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Azam FC, jana Jumanne aliungana na wenzake katika kambi yao nchini Afrika Kusini ambapo katika nafasi yake hiyo, atakuwa na kazi kubwa ya kupambana na Said Mohammed ‘Nduda’.
Akizungumza na Gazeti la Championi, Manula alisema kuwa: “Niwashukuru watu wote ambao nilifanya nao kazi ndani ya Azam, wao wamenilea mpaka leo hii nimekuwa hivi, siwezi kuacha kuwashukuru, kwa sasa mimi ni mchezaji wa Simba, hivyo nguvu zangu zote nazihamishia huku.
“Wanasimba wanipokee vizuri na wategemee mengi mazuri kutoka kwangu, nimekuja huku kwa malengo mengi ikiwemo kuifanya Simba ipate mataji mengi zaidi na tufanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa, naamini kuwa tuna timu bora,” alisema Manula.
Post A Comment: