Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema ikiwa atashindwa kwa haki, Uchaguzi Mkuu wa tarehe nane mwezi Agosti, atakubali matokeo na kukabidhi madaraka kwa amani.
Rais Kenyatta ametoa hakikisho hilo wakati akijibu maswali mbalimbali kupitia runinga na kumtaka mpinzani wake Raila Odinga, naye kuwa tayari kufanya hivyo ikiwa atashindwa katika Uchaguzi huo.
Kenyatta amesisitiza kwamba, yeye ni mtu anayeheshimu uamuzi wa wananchi, na kuwaomba wapinzani wake nao wafanye hivyo.
Aidha, amesema serikali yake imelenga Uchaguzi huo uwe wa amani ndiyo maana maafisa wa usalama wamejihami na wako tayari kukabiliana na wale watakaotaka kuzua fujo.
Naye Bw. Odinga, anayepeperusha bendera ya muungano wa upinzani NASA, amekuwa akisema kuwa atakubali matokeo hayo ikiwa Uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Hata hivyo, hivi karibuni ametoa madai mazito kuwa Rais Kenyatta anatumia jeshi kumsaidia kuiba kura, madai ambayo serikali imekanusha.
Post A Comment: