ads

MWANAFUNZI bora wa kike, Sophia Richard Juma (18) aliyeongoza ufaulu wa masomo ya sayansi katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka huu amesema amepania kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na kwamba kiu yake kubwa ni kuonana na Rais John Magufuli ili amshike mkono kwa nia ya kumpongeza.


Aidha, kinara wa masomo ya mchepuo wa Lugha na Sanaa, ambaye ni wa EGM (Uchumi, Jiografia na Hisabati), Francis Samkyi wa Shule ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam, alisema amefurahi kutimiza lengo la mtihani huo na kwamba sasa nia yake ni kutimiza ndoto yake ya kuwa mtaalamu wa masuala ya fedha.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana mjini Zanzibar na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Musonde, Sophia alikuwa kinara wa masomo ya sayansi, akifuatiwa na Agatha Ninga wa Tabora Girls ya Tabora na Nathaniel Ndagiwe wa Mzumbe ya Morogoro.

Samkyi aliibuka kidedea katika masomo ya lugha na sanaa, akifuatiwa na Jophary Ernest na Andrea Nkondo, wote wa Ilboru ya Arusha.

Katika orodha hiyo ya wanafunzi waliong’ara kwa kila mchepuo, Rajabu Ali Mabaranga wa shile ya Kibaha mkoani Pwani aliongoza katika msomo ya biashara, akifuatiwa na Gasto Theobalo Kimaro wa Umbwe ya Kilimanjaro na Rashid Abdallah wa Tusiime ya jijini Dar es Salaam.

SOPHIA ALIVYOMTAJA JPM

Sophia amehitimu shule ya sekondari St. Mary’s Mazinde Juu iliyopo Lushoto mkoani Tanga, akisomea mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).

Pia ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne wa familia ya Richard Tadeo na Joyce Ezra, wakazi wa Pasiansi wilayani Ilemela, mkoa wa Mwanza ambao shughuli zao kuu ni uvuvi. Kabla ya kwenda kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kambi ya Msange mkoani Tabora, ambako kwa sasa ndipo alipo, Sophia aliwaahidi wazazi wake, kwamba mwaka huu atatenda maajabu yatakayompa fursa ya kushikana mkono na rais Magufuli.

Akizungumza na gazeti la Nipashe kwa njia ya simu jana, mama wa Sophia, Joyce Ezra, alisema licha ya kumsomesha mtoto wao kwa shida ikiwamo kukopa fedha kila mara ili wamlipie ada, matokeo hayo yaliyotangazwa na NECTA na mwanawe (Sophia) kuongoza kitaifa katika masomo ya sayansi, wanaona wazi kwamba amewatendea haki na pia kutimiza kile alichowaahidi.

“Kila tulipokuwa tunaenda kukopa fedha, tulimuonyesha na kumwambia tumekopa fedha, tusije tukafungwa bure… jitahidi maana tulijinyima na hata wakati mwingine kulala njaa ili mtoto wetu asome,” alisema Joyce.

“Mara kwa mara amekuwa akituambia kwamba anataka kuwa daktari bingwa wa moyo ili aweze kutibu watu. Lakini kikubwa zaidi ni kwamba mwaka huu alijitabiria kuwa mwanafunzi bora na kwamba naamini kwa kufanya hivyo atapata fursa ya kuonana na kupeana mkono na Rais John Magufuli,” alisema mama huyo wa Sophia jana.

Kwa kawaida, wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya taifa hupata nafasi ya kwenda bungeni na kupongezwa huku pia wakitunukiwa zawadi mbalimbali.

Akimuelezea Sophia, mama huyo alisema kuwa alisoma katika Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Mwanza, kisha kusoma sekondari shule ya wasichana Visitation iliyopo Moshi mkoa wa Kilimanjaro.

Credit - Nipashe
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: