Rais John Magufuli amemtaka Mbunge wa Morogoro mjini (CCM) Aziz Abood kurejesha viwanda alivyobinafsishiwa na serikali kama ameshindwa kuviendesha ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.
"Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwamo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwamo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira… nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu," alisema Rais Magufuli.
Magufuli ametoa agizo baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kuelekea jijini Dar Es Salaam kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu na kumueleza kero ya kunyanyaswa na maofisa wa Manispaa, ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada ya kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, amewaagiza viongozi wa manispaa hiyo na viongozi wa mkoa kuwaacha wafanyabiashara ndogo ndogo wa mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.
Post A Comment: