ads

Rais John Magufuli amekuwa akiruhusu wananchi wanaobeba mabango yaliyoandikwa kero zao na kuyasoma kwa sauti kwenye kipaza sauti, lakini sasa anaonekana kuyachoka.


Na jana aliwataka wananchi wa Tabora wayashushe ili aendelee na hotuba yake, ikiwa ni siku moja baada ya kuwaambia wakazi wa Kigoma kuwa ameshayaona mabango yao na atayafanyia kazi.

Jana wananchi waliyanyanyua juu mabango hayo mara baada ya Rais kupanda jukwaani kuhutubia, hali iliyomlazimu kusimamisha hotuba yake.

“Naomba mshushe hayo mabango ili niendelee na hotuba yangu,” alisema Rais lakini wananchi waliendelea kunyoosha mabango hayo, hali iliyoonyesha kumkera zaidi.

“Nimesema shusheni hayo mabango, la sivyo siwezi kuyashughulikia. Mkitoka hapa nendeni mkayatandike nyumbani kwenu.”

Mabango hayo yamekuwa yakieleza matatizo ambao wananchi wanakumbana nayo katika maeneo yao, badala ya matatizo yanayozungumzwa jukwaani. Baadhi ya matatizo hayo ni pamoja na kero za mirathi, kuporwa ardhi na kubambikiwa kesi.

Hata hivyo, Rais aliamua kusoma mabango hayo mwishoni mwa hotuba yake, huku akitoa ufafanuzi.

“Sitaki kukuita mtu wa ardhi hapa, lakini tambua kwamba mabango yote nimeshayapiga picha yapo kwenye CD yangu nitaenda kuangalia Dar es Salaam,” alisema huku akitoa maelekezo ya viongozi waliohodhi ardhi kuiachia mara moja.

Hata baada ya kushusha mabango hayo, upande mwingine wananchi walionekana kunyanyua viti juu hali iliyosababisha Rais kusitisha tena hotuba yake na kuwataka washushe viti hivyo.

Katika hatua nyingine Rais amesema ataendelea kuteua viongozi wenye uwezo kutoka vyama vya upinzani ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

Magufuli aliyasema hayo jana katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi wakati akiwahutubia wananchi wa Tabora baada ya kuzindua miradi yenye thamani ya Sh457.256 bilioni ikiwemo barabara yenye umbali wa kilomita 114.9 kutoka Tabora mpaka Nzega.

Alitoa mfano wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, akisema aliamua kumteua kwa kuwa aliona ana uwezo wa kufanya kazi, hivyo hakuwa na sababu ya kuangalia alitokea chama gani.

“Nitaendelea kuwachomoa wenye akili kutoka vyama vingine. Wale vilaza vilaza waliopo kwenye vyama hivyo wataendelea kuwepo huko. Watanzania wanahitaji maendeleo, wamechoka kuzungushwa na masuala ya siasa kila siku,” alisema Magufuli.

“Mimi ni Rais wa watu wote, hata ukitaka niwepo wapi, nitasomba wote na kila mwenye uwezo wa kuongoza ataongoza haitajalisha kabila, chama, rangi na vinginevyo, ilimradi ana uwezo atapata nafasi kwenye serikali yangu.”

Hotuba yake iligusa mambo tofauti ambayo amekuwa akiyasema kila anaposimama kuhutubia kama wafanyakazi hewa, ufisadi, ukwepaji kodi, kuondoa kodi za kero na uboreshaji usafiri.

Jana, alitumia hotuba hiyo kumsifu Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye anasifika kwa kuunganisha mikoa mingi kwa barabara ya lami.

“JK asingekubali kuanzisha miradi hii ya ujenzi, nisingeweza kuanzisha. Mimi nilikuwa chini yake na yeye alikuwa Rais, alianzisha miradi ya ujenzi wa barabara kwa kutumia fedha za ndani. Wakati huo wafadhili walikuwa wamegoma kutoa misaada kwa ajili ya miradi hii,” alisema Magufuli.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: