Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama kiongozi.
Hata hivyo, Profesa Lipumba amemtaka arejee ofisini kuendelea na majukumu yake licha ya kudai kwamba kwa sasa nafasi yake inakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya.
Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni jana, Profesa Lipumba amesema bado anamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu wa chama hicho licha ya utoro wake kazini.
"Sijamwona Katibu Mkuu tangu Septemba 23 mwaka jana, namkaribisha aje ofisini Buguruni apokee maelekezo kutoka kwa mwenyekiti," amesema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti huyo amesisitiza kwamba yeye ni mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa ibara ya 117 ya chama hicho ambayo inaeleza taratibu za kiongozi kujiuzulu.
"Ibara ya 117 inatoa mamlaka kwa mkutano mkuu kujadili barua ya kiongozi kisha kuridhia kujiuzulu kwake au laa. Sasa mimi niliandika barua ya kutengua kujiuzulu kwangu kabla mkutano mkuu wa chama haujakaa kuijadili barua yangu ya kujiuzulu," amesema.
Post A Comment: