ads

SIKU tano baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuikabidhi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mgawo wa Sh. milioni 40.4 zinazodaiwa kuwa zao la kashfa ya uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow,'mhenga' mwingine aliyekuwa mstari wa mbele kuvalia njuga sakata hilo, Kangi Lugola, ameibuka na kuwajia juu wanufaika wengine.


Awali, kwa nyakati tofauti, vinara wengine katika kufichua sakata hilo bungeni walitoa maoni yao mbalimbali kuhusiana na hatua ya Ngeleja, baadhi yao wakiwa ni mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila; Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Hivi karibuni, neno ‘mhenga’ limejitwalia umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, likihusishwa na maana isiyo rasmi ya kuwaelezea magwiji au waasisi wa jambo au dhana fulani.

Akizungumza na gazeti la  Nipashe jana, Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) aliyekuwa pia akipinga vikali kile kilichotokea katika kashfa ya fedha za Escrow, alimpongeza Ngeleja kwa hatua aliyoichukua na kuwataka wanufaika wengine wa mgawo wa fedha zinazohusishwa na Escrow wafuate nyayo zake, baadhi yao ni aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu, Andrew Chenge na aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika serikali ya awamu ya nne, Prof. Anna Tibaijuka. Wote wawili walidaiwa kupata Sh. bilioni 1.6 kila mmoja.

Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya nne, Jumatatu alitangaza kukabidhi mgawo wake TRA, uamuzi uliowaibua Lissu (Chadema), Zitto (ACT-Wazalendo) na Kafulila, ambao walisema Ngeleja amethibitisha kuwa anastahili kukamatwa na kushtakiwa pamoja na watu wote waliopata mgawo huo.

Hata hivyo, Lugola alimpongeza Ngeleja kwa uamuzi wake kuwataka wanufaika wengine wote warejeshe fedha walizopewa serikalini.

Lugola alisema wakati wakipambana ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuitaka serikali ya awamu ya nne kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa, walionekana hawako sahihi.

Alisema anaamini kuwa kitendo cha Rais John Magufuli kuibua suala hilo ndicho kilichomfanya Ngeleja kurejesha fedha hizo baada
ya kuona hatua zimeanza kuchukuliwa.

“Nina mawazo matatu kwa nini Ngeleja amerejesha fedha," alisema Lugola.

"Mosi; unaweza kuomba fedha kwa mtu au kampuni akakupa, lakini usijue chanzo chake. Ni sawa na mtu anapotoa sadaka kanisani Padri hakuulizi chanzo cha fedha ndipo utoe sadaka.

“Pili; unaweza kujua kuna shughuli fulani imefanyika sasa ndiyo unapewa mgawo wako, lakini tatu kwenye benki zipo fedha zinaingizwa kwenye akaunti za watu pasipo mmiliki wa akaunti kuhusishwa, wanaoziona fedha za aina hii ni asilimia mbili tu huuliza benki husika, lakini asilimia iliyobaki huona kama bingo imeingia."

Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatatu, Ngeleja alisema fedha hizo aliziomba kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kijamii jimboni kwake.

“Yeye alisema aliziomba kwa ajili ya jimbo lake, swali kwanini anazirudisha?" Alihoji Lugola.

"Kwa mtazamo wangu, labda wakati akiziomba hakujua zimetokana na nini na kwa bahati nzuri au mbaya, kipindi kile zilisafishwa, ila awamu hii imechukua hatua, Ngeleja ameona fedha alizopewa zina matatizo, ameamua kuzirejesha serikalini."

Alisema hatua iliyochukuliwa na mbunge huyo ni ya kiungwana na inapaswa kufanywa na wanufaika wengine wa mgawo huo kwa kuwa huu ni muda mwafaka kwao kuzirejesha.

“Ngeleja amewafungulia njia… njia ni nyeupe. Rudisheni hizo fedha hata kwa wale walioziita hela ya mboga, kwao ni ya kitoweo, sisi tutaitumia kujengea madarasa, kuweni wajasiri kama Ngeleja zirudisheni,” alisema, akielekeza ushauri wake kwa waliodaiwa kunufaika.

Ripoti iliyowasilishwa katika kikao cha 18 cha Bunge la 10 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliainisha majina ya maofisa wa serikali, wabunge na viongozi wa dini waliopata mgawo wa fedha hizo.

Watu hao walipewa fedha hizo na Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza kwa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Mkurugenzi huyo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Power African (T) Limited (PAP), Habinder Sethi Sigh wako mahabusu kwenye Gereza la Keko jijini Dar es Salaam baada ya kunyimwa dhamana wiki iliyopita walipofikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka 12, yakiwamo ya kuhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4.

Kwa mujibu wa ripoti, mbali na Chenge na Tibaijuka, watu wengine waliotajwa kupata mgawo huo ni ofisa katika Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh. milioni 80, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa Sh. milioni 404.25 na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) Dk. Enos Bukuku Sh. milioni 161.7.

Katika ripoti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Aloisius Mujulizi, walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.

Wengine ni Ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko Sh. milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius Nzigirwa milioni 40, Padri Alphonce Twimanye Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita, Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.

Credit - Nipashe
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: