Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kusema ukweli na kudai katika mambo ambayo yeye hayapendi basi ni ubinafsishaji na ameamua kusema hilo kwa uwazi ili hata waliofanya jambo hilo wajue kuwa walifanya dhambi kwa Watanzania
Rais Magufuli amesema hayo leo alipokuwa kwenye mkoani Singida wakati akizindua barabara ya Manyoni- Itigi na Chaya barabara yenye urefu wa kilomita 89.3 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami. Rais Magufuli amesema kuwa jambo la ubinafsishaji limeirudisha nyuma nchi kimaendeleo na kufanya viwanda vingi vimekufa.
Aidhaa Rais Magufuli amesema Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa na lengo lake ni kuona inakuwa kama Ulaya ili ifike wakati Tanzania iwe inatoa msaada Ulaya
"Nataka hii Tanzania iwe Ulaya na tutafika lakini kabla ya kufika huko tutabanana kweli kweli na watu wakubali kubanana ili tufike huko, maana tusipochukuliana hatua sisi wenyewe hatutafika mahali tunapotaka badala ya sisi kuwa tunabembeleza misaada nataka sisi tuwe tunatoa misaada kwao huko mbeleni. Nataka tuwe tunatengeneza nguo tunavaa kwanza baadaye tunawapelekea Ulaya wakavae mitumba maana pamba ni yetu sisi, haiingii akilini pamba ya kwetu tunapeleka kwao wanatengenza nguo wanavaa na kuleta mitumba kwetu nataka hiyo ibadilike tunatengeneza sisi wao wakavae mitumba kutoka hapa" alisistiza Magufuli
Rais Magufuli anasema hayo ndiyo yalikuwa malengo ya baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiyo maana aliweza kujenga viwanda vingi ili kuzalisha vitu hapa lakini mawazo hayo yamekuja kufa kutokana na ubinafsishaji.
"Ndiyo maana mimi suala la ubinafsishwaji silipendi siwezi kuwalaumu waliofanya lakini sitaacha kusema, katika viwanda zaidi ya 100 vilivyobinafsishwa saizi viwanda 97 yamebaki kuwa magodauni, walitudanganya hao hao wazungu tuingie ubinafsishaji wakati wao hawafanyi hivyo, sisi kila kitu tunafanya ubia na matapeli, wengine watasema huyu Rais kwanini anasema hivi jamanii lazima niyatapike sababu nikibaki nayo nitapata 'pressure' na nikitapika wale waliofanya lazima wakumbuke kwamba kuna mtu anatapika dhambi zao" alisema Magufuli
Mwaka 1993 Tanzania ilianza kutekeleza sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma vikiwemo viwanda ambapo ilisema kuwa imeamua kujitoa katika uendeshaji wa biashara jambo ambalo lilipelekea viwanda vingi kufungwa kutokana na wawekezaji kushindwa kuviendesha. Kwa mujibu wa hotuba ya Upinzani Jumla ya mashirika 374 yalibinafsishwa yakiwemo ya Kilimo 95, Viwanda 94, miundombinu 23, Maliasili 34 , Nishati 15 ambapo viwanda mbalimbali vilifungwa.
Post A Comment: