Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imefanikiwa kuongeza mapato yake, kutoka Sh56 bilioni kwa miaka minne iliyopita hadi kufikia Sh90 bilioni mwaka 2016/17 kutokana na watalii ambao wametembelea hifadhi hiyo.
Mataifa ambayo yanaongoza kuleta watalii wengi wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro ni Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.
Kutokana na takwimu za mwaka 2015, watalii 67,583 walitoka Marekani, 41,691 wametoka Uingereza, 37,744 wanatoka Ujerumani wakati watalii 25,240 wanatoka Ufaransa.
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fredy Manongi akizungumza na Mwananchi juzi, amesema kuongezeka mapato hayo, kumetokana na kazi kubwa iliyofanywa kuitangaza Tanzania nje ya nchi na pia kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya mamlaka hiyo.
Amesema kwa sasa mamlaka hiyo, inapata wastani wa watalii 600,000 kwa mwaka na wamekuwa wakiendelea kuongezeka kutokana na kazi kubwa ya kutangaza vivutio vya utalii inayofanywa na mamlaka hiyo, Serikali na wadau wa utalii.
Amesema tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa pia idadi ya watalii wa ndani, wanaotembelea hifadhi hiyo, imeanza kuongezeka na kukaribia kuwa sawa na watalii wa nje.
“Kwa sasa tumeanza kupokea watalii wengi wa ndani hasa nyakati za sikukuu na tunaimani Watanzania wengi zaidi wataendelea kujitokeza kutembelea hifadhi hiyo,”amesema.
Hata hivyo, Dk Manongi amesema tatizo kubwa linalowakabili watalii wa ndani kushindwa kutembelea vivutio vya utalii ni gharama ya usafiri na si malipo ya Sh10,000 wanayotozwa wanapotembelea hifadhi hiyo.
Awali Kaimu Meneja Uhusiano wa NCAA, Vincet Mbilika amesema, mamlaka hiyo imejipanga kuwa na mikakati maalum ya kuhamasisha utalii wa ndani ili Watanzania wengi wafike kuona maajabu ya Ngorongoro.
Amesema katika hifadhi hiyo ambayo ni moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika, ni rahisi zaidi kuona wanyama wote wakubwa kama tembo, faru, simba, nyati na chui katika eneo la Kreta ya Ngorongoro na maeneo mengine yaliyohifadhiwa.
Mamlaka ya hifadhi hiyo, pia ni moja ya maeneo ya urithi wa Dunia, yaliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) kutokana na kuwa na sifa za kipekee, ikiwepo kreta pamoja na wanyama na watu jamii ya kimasai kuishi pamoja.
Post A Comment: