Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu, amemshukia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na kumtaka kuacha unafiki kuhusu futari yake aliyoandaa na kususiwa na wabunge wa upinzani.
Lisu amesema kuwa hawezi kushiriki kwenye futari ya Spika Ndugai au kiongozi yeyote wa CCM kwa sababu wameamua kuwabagua na kuwadhalilisha.
Maneno hayo ya Lisu yamekuja ikiwa ni siku chache tangu Spika Ndugai alipoeleza kuhusu madai ya upinzani kupanga kususia futari yake aliyoandaa Jumanne wiki hii na kusema kuwa jambo hilo si zuri kwani kuna umuhimu wa jamii kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao.
Ndugai alielezea pia wabunge wa upinzani walisusia futari iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema kuwa inapofika hatua ya kutoshirikiana katika masuala ya kijamii inakuwa sio vizuri sana.
Lisu alisema kuwa kiongozi huyo amekuwa akiwadhalilisha na kutoa adhabu za vifungo vya nje ya Bunge huku akiwazuia kutoa mawazo mbadala ndani ya Bunge.
"Kiongozi anayewabagua namna hii bungeni, unawezaje kwenda kwenye futari au shughuli yake? Aache unafiki kwa lengo la kutaka kuonekana mwema machoni mwa jamii".
Aidha, Lisu alienda mbali na kusema kuwa Ndugai amebinafisisha shughuli za Bunge kwa serikali na kwamba kwa sasa anafanyakazi kwa kushirikiana na serikali badala ya bunge kubaki lifanye shughuli za kibunge.
Post A Comment: