Ni Bajeti ya mageuzi na huduma bora kwa jamii. Hayo ni maneno machache ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Khalid Salum Mohamed aliyoyatoa jana wakati akimalizia uwasilishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka 2017-2018.
Akiwasilisha bajeti hiyo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Waziri Dk Khalid aliomba kuidhinishiwa Sh1.84 trilioni kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema kwamba Sh324.7bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi wa Serikali, Sh64.3 bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya ruzuku kiutendaji na Sh101.7 bilioni kwa ajili ya matumizi mengine ya kazi za kawaida.
Aliongeza kuwa, Sh100 bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya mfuko wa maendeleo na Sh116 bilioni ni michango ya matumizi ya maendeleo.
“Lakini pia Serikali imetenga Sh10 bilioni ambazo zitatumika kwa ajili ya malipo ya ziada ya pensheni kwa mwaka ujao wa fedha wa 2017-2018, hivi sasa tupo katika mchakato wa kugawa fedha hizo na mpango wa malipo hayo utatangazwa baada ya mchakato huo kukamilika,” alisema. Alisema kuwa kiwango hicho cha bajeti yenye ongezeko la asilimia 6.8 cha makusanyo ya kodi za ndani ni kikubwa ukilinganisha na Sh841.5bilioni za 2016/17.
Alisema bajeti hii inaonyesha kiwango cha utegemezi wa fedha za wafadhili kimeshuka.
Alisema kuwa Sh590.8 bilioni zitatumika kwa kazi za kawaida na Sh496.6 bilioni zitatumika katika kazi za maendeleo kwa mwaka huo wa 2017/18.
Dk Khalid alisema miongoni mwa fedha zinazotarajiwa kutumika mwaka huu ni Sh675.8 bilioni zinazotarajiwa kukusanywa katika vyanzo vya ndani, ikiwamo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ambayo imepangiwa kukusanya Sh347.3 bilioni na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nayo inakadiriwa kukusanya Sh258.7 bilioni kutokana na mapato ya kodi huku mapato mengine kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato vya Serikali yakikadiriwa kufikia Sh69.8 bilioni.
Dk Khalid alisema mbali ya mapato hayo, Serikali inatarajia kupokea pia Sh380.5bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Alisema kati ya fedha hizo ipo ruzuku ambayo ni Sh82.2 bilioni pamoja na Sh298.3 bilioni zitakazopatikana kwa njia ya mikopo.“Uchumi wa Zanzibar bado unaendelea kuimarika ukilinganishwa na wastani wa viwango vya kasi ya ukuaji uchumi kwa nchi za Kanda ya Afrika Mashariki na zile zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema Dk Khalid.
Alisema kwamba kwa mwaka 2016, pato halisi la Taifa lilifikia Sh1,628 bilioni ikilinganishwa na Sh1,188 bilioni kwa mwaka 2015, sawa na kasi ya ukuaji wa asilimia 6.8.
Post A Comment: