Tanzania imeendelea kudhibiti kiwango cha mfumuko wa bei katika kipindi cha miaka minne mfululizo huku kukiwa na matumaini ya hali hiyo kuendelea kupungua kutokana na mikakati inayoendelea kuchukuliwa na Serikali.
Akisoma hali ya uchumi nchini bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango ameeleza kuwa kiwango cha mfumuko huo katika kipindi cha mwaka 2016 kilikuwa asilimia 5.2, kikiwa kimeshuka kwa alama chache ikilinganishwa na kile kilichorekodiwa mwaka mmoja nyuma (2015) kilichokuwa asilimia 5.6.
Amesema kuimarika kwa kiwango hicho kulichangiwa na mambo kama kukua kwa biashara ya mafuta katika soko la kimataifa, kuwepo kwa uhakika wa chakula na sera madhubuti zinazotekelezwa na Serikali.
Hata hivyo, Dk Mpango amesema hali ya mfumuko wa bei iliongezeka na kufikia asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ikichangiwa na ukosefu wa mvua.
“ Wananchi wengi waliingiwa na hofu kwamba kungekuwa na tatizo la ukosefu wa chakula hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya chakula,” amesema.
Hata hivyo, amesema kiwango hicho cha mfumuko wa bei kimeshuka kuanzia Mei na kufikia wastani wa asilimia 6.1.
Post A Comment: