NEEMA imeanza kunukia Yanga baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kudaiwa kurejea kimya kimya ili kuinusuru timu hiyo katika kipindi hiki cha usajili. Taarifa za ndani kutoka Yanga zinadai kuna uwezekano mkubwa wa kurejea kwa Manji baada ya wanachama kumuomba.
Manji alitangaza kujiuzulu karibuni na mara kadhaa wanachama wa Yanga wamemwomba arudi ili kuinusuru na ukata. Tangu ajiuzulu, Yanga imekuwa katika wakati mgumu kifedha kutokana na kumtegemea kwa asilimia kubwa katika masuala mbalimbali hasa katika usajili.
Taarifa za ndani ya Yanga zinadai Manji amerejea kimya kimya na kufanya usajili wa mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu na wachezaji wengine maarufu waliopo. Mbali na Ajibu, inadaiwa kawashawishi pia mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Thaban Kamusoko waendelee kuchezea Yanga baada ya mikataba yao kumalizika.
Mwenyekiti huyo anadaiwa kurejea huku kukiwa na habari kuwa, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima amesajiliwa Simba ingawa awali alikiri kuwa atabaki Yanga. Mchezaji ambaye pia hana uhakika wa kurudi Yanga ni mshambuliaji Amis Tambwe aliyemaliza mkataba wake.
Alipoulizwa kuhusu Manji kudaiwa kurejea na kusajili, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema hana taarifa hizo wala za usajili wa Ajibu. “Sina hizo taarifa lakini watu waendelee kusubiri huwezi jua nini kitatokea mbele. Kuhusu usajili tunaendelea na kama kuna taarifa tutawaeleza,” alisema Mkwasa.
Mkwasa aliwataka mashabiki wasiwe na wasiwasi kuhusu usajili wanaofanya kimyakimya na muda si mrefu kuna mambo makubwa ya kushangaza yanakuja Yanga. Kauli ya Mkwasa imetafsiriwa kuwa inaashiria kurejea kwa Manji ingawa hapendi kuweka wazi juu ya kauli hiyo.
Juzi Yanga ilifanikiwa kumnasa beki wa Jang’ombe Boys ya Zanzibar, Abdallah Shaibu Ninja na kuwabakisha beki Nadir Haroub Cannavaro na Niyonzima. Hata hivyo, haikusema nani kalipia usajili wao.
Mkwasa amesema ukimya wao kwenye usajili hautokani na ukata bali ni utaratibu mpya waliojiwekea kutowapa nafasi wapinzani kujua wachezaji wanaowasajili. Mkwasa alisema kikosi chao hakihitaji marekebisho makubwa kama ambavyo wengine wanadhani ndiyo maana wako kimya wakiangalia wachezaji sahihi ambao wataweza kutimiza kile wanachokihitaji.
“Ukimya wetu una maana na siyo kwamba tuna tatizo la pesa. Tuna fungu la kutosha kufanya usajili ila tunafuata kile ambacho kimeelekezwa kwenye ripoti ya kocha hasa ukizingatia kikosi chetu kinahitaji marekebisho madogo,” alisema Mkwasa.
Alisema kilichowachelewesha kuanza zoezi la usajili ni kuwaongeza mikataba baadhi ya wachezaji wao nyota ambao mikataba yao ya awali ilifikia mwisho msimu huu. Alisema tayari wamekamilisha kazi hiyo kwa baadhi ya wachezaji na wengine watafanya hivyo wakirudi nchini kutoka michuano ya kimataifa wanayoshiriki.
Alisema wamekusudia kutompoteza mchezaji wao hata mmoja ambaye wanamhitaji na hilo limefanikiwa baada ya wachezaji wote kukamilisha mazungumzo na kilichobaki ni kusaini mikataba mipya.
Post A Comment: