Baba mzazi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Elisha Mghwira (87) amesema taarifa za kuteuliwa kwa binti yake na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo amezipokea kwa furaha na kwamba zitamwongezea muda wa kuishi.
Anna ambaye alikuwa mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, aliteuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli kujaza nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki aliyejiuzulu.
Akizungumza na gazeti la Mwananchi nyumbani kwake katika Kata ya Kibaoni mjini hapa jana, mzee Mghwira alimtaka mwanaye kuendeleza uadilifu alionao ili asimwangushe kiongozi aliyemteua.
“Ingawa kumbukumbu nyingi nimeanza kuzisahau kutokana na uzee wangu, lakini niujuavyo Mkoa wa Kilimanjaro ni mkoa wenye wasomi wengi kuliko mkoa wetu wa Singida na mikoa mingine mingi,” alisema.
Aliongeza: “Kwa hiyo, mtoto wangu Anna ana mtihani mkubwa katika kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, lakini Mungu atamtangulia aweze kuwatumikia vyema.”
Alisema Anna ni mtoto wake wa tatu kati ya watoto tisa na kwamba, amekuwa na bidii ya kujisomea kuanzia shule ya msingi, ni mchapakazi asiye na rekodi ya udanganyifu.
Akizungumzia uteuzi huo kanisani jana, Askofu wa Kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida Mjini, Dk Paulo Samwel aliwataka wazazi mkoani humo kuwasomesha watoto wao wa kike ili mkoa huo uweze kutoa viongozi wengi zaidi.
“Tukiwa na wasomi wazuri wa kike ipo siku mkoa wetu wa Singida utatoa kiongozi wa ngazi ya juu zaidi ya ukuu wa mkoa. Namshukuru Dk Magufuli kwa kumteua Anna Mghwira nina uhakika hatajutia uamuzi wake,” alisema.
Ametoa wito kwa wanaume wanaosababisha watoto wa kike kutotimiza ndoto zao kielimu kwa kuwabebesha mimba wafichuliwe ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Credit - Mwananchi
Post A Comment: