Mwenyekiti wa Kamati ya Pili iliyofanya uchunguzi wa usafirishaji wa mchanga wa madini, Profesa Nehemiah Osoro amesema kampuni inayomiliki migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, haina sifa za kufanya shughuli za uchimbaji wa madini hapa nchini.
Profesa Osoro ametoa kauli hiyo leo Jumatatu alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo Ikulu jijini Dar es Slaam. Kamati hiyo inawasilisha ripoti hiyo ikiwa siku 18 zimepita tangu Rais apokee ripoti ya kwanza iliyoeleza kwamba, Taifa linaibiwa kupitia usafirishaji wa mchanga huo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli alitengua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kuvunja bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) na kumsimamisha kazi mkurugenzi wa bodi hiyo.
Kamati inayowasilisha taarifa yake leo iliteuliwa na Rais na ilipewa hadidu mbalimbali ikiwamo kufanya tathmini ya usafirishaji wa mchanga huo iwapo ulizingatia mikataba ya MDAs, kuangalia kama maslahi ya Taifa yalizingatiwa, kubaini idadi ya makontena yaliyosafirishwa tangu mwaka 1998.
"Matokeo ya uchunguzi huu yanaonyesha kuwa kampuni ya Acacia haina sifa za kuchimba wala kufanya biashara ya madini hapa nchini, inafanya shughuli zake kinyume cha sheria za nchi, hii inashangaza sana,"alisema.
Post A Comment: