ads

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema timu aliyoiunda ichunguze tuhuma za ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) imekamilisha kazi yake na imebaini madudu mengi zaidi.


Machi 16, 2017, Waziri Mkuu aliivunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma. 

Alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora awakamate viongozi wanne wa pamoja na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Waziri Mkuu ambaye amefanya ziara ya siku moja mkoani Tabora, ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 15, 2017) wakati akizungumza na wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa wadau wa zao la tumbaku katika ukumbi wa Kiyungi mwana Isike, mjini Tabora.

“Nilikuja Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo nimekuja kuendelea na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwezesha kilimo cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima, wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na viongozi wa Serikali wawepo kwenye mkutano huu,” amesema.

Akitoa mrejesho juu ya uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda, Waziri Mkuu amesema WETCU haikuwa na kitengo cha ununuzi kwa zabuni.

“Waliunda kampuni inayoitwa FDTU (Flu and Dark Tobacco Union) ambayo ni Umoja wa Wenyeviti wa Union zote za Tumbaku nchini ambayo ilipewa kazi zote za ununuzi wa pembejeo na hela walikuwa wanagawana,”amesema.

“Tumefanya ufuatiliaji hadi katika benki lakini kwenye akaunti hakuna hela mpaka sasa. Tumeangalia chanzo cha fedha za union zenu na kubaini hakuna fedha zinazotoka FDTU kwenda WETCU,” ameongeza.

Akifafanua kuhusu kashfa ya ununuzi wa gari aina ya shangingi lenye namba za usajili T181 DEN ambao ulifanywa kinyume na maazimio ya mkutano mkuu, Waziri Mkuu amesema viongozi wa WETCU walitumia zaidi ya sh. milioni 220 kuzidi kiwango kilichoidhinishwa na Mkutano Mkuu cha kununua gari lenye thamani ya sh. milioni 40.

“Gari walilolinunua ni la mwaka 2008 na siyo la mwaka 2015 kama taarifa zinavyoonesha. Lilikwishatumika kwa kilometa zaidi ya 95,000 lakini likarekebishwa hadi kubakiza kilometa 16,000 ili lionekane ni jipya,… maana yake wamekula fedha nyingi sana na ni lazima tuwachukulie hatua za kisheria kwa sababu wamekula fedha, wamenunua gari lililotumika na siyo maamuzi ya mkutano mkuu.”

Waziri Mkuu ameagiza Mkurugenzi wa kampuni ya 4×4 Tanzania Limited, Bw. Faraz Yaseen naye akamatwe na kuhojiwa ni kwa nini alihusika na kuuza gari la mwaka 2008 lakini akabadilisha nyaraka ili lionekane ni la mwaka 2015.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uuzaji wa hisa za WETCU, Waziri Mkuu amesema chama hicho kilikuwa na hisa milioni 36 ambapo kilitoa milioni sita ili ziuzwe na zikapatikana sh. bilioni 2.520 na ndiko huko walitoa fedha za kununulia gari na vifaa vya ofisi kwa sh. milioni 49.

“Walichukua hisa 100,000 na kuziuza na wakapata sh. milioni 250 lakini fedha hizo hazikuwekwa kwenye akaunti ya chama. Hisa zilizobakia, ambazo ni milioni 30, walishaanza mchakato wa kuuza hisa milioni 28. Je mliahsatoa kibali Wamempatia cheti halisi cha hisa hizo wakala Zani Security ili auze hisa hizo bila kuomba kibali cha Mkutano Mkuu,” amesema.

“Kwa vile hawakupata idhini ya Mkutano Mkuu, na wala hawakufuata taratibu, kanuni na sheria, kuanzia leo nimesitisha mauzo ya hisa hizo na kirudishwe Tabora mapema iwezekanavyo. Mrajisi fuatilia Zani Securiy warudishe kile cheti kinachowapa dhamana ya kuuza hizo hisa.”

Waziri Mkuu amesema, kwa vile WETCU ina madeni mengi katika benko za CRDB na NMB, viongozi wa chama hicho waliamua kufungua akaunti mpya za fedha za kitanzania na dola za Marekani kwenye benki ya EXIM. Walifungua akaunti ya muda maalum na kuweka huko fedha ambazo zilishalisha faida ya zaidi ya sh. milioni 14 katika kipindi cha miezi mitatu.

“Ninamuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kupitia COASCO (Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika) ya Tabora afuatilie benki ya EXIM hapa Tabora ili kubaini ni akina nani walikuwa wakifanya miamala hiyo,” amesema,

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba; Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri za mkoa huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA,
JUMAMOSI, APRILI 15, 2017
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: