Katika hali isiyo ya kawaida,wananchi wa Kijiji cha Majengo, kilichopo kwenye Jimbo la Mtama, mkoani Lindi ambao ni Waislamu, wiki iliyopita waliangusha dua ndani ya Kanisa Katoliki Parokia ya Nyangao, ili kumtakia afya njema Mbunge wao, Nape Nnauye katika kazi zake za ubunge.
Nape, akiwa ameambatana na baadhi ya waigizaji wa filamu na wachekeshaji, alikuwa amekwenda jimboni kwake Mtama, kuzungumza na wapiga kura wake, ikiwa ni mara ya kwanza tangu nafasi yake ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo itenguliwe na Rais Dk. John Pombe Magufuli, mwezi uliopita.
Ndani ya kanisa hilo, ambamo pia walikuwepo waumini wa Kikristo, bila kujali tofauti zao, Waislamu hao walisoma dua kwa ajili ya kumtia nguvu ya kuwatumikia wananchi wake na kumtaka kutokata tamaa katika utendaji wa kazi zake za kibunge, kwani kilichotokea ni kitu cha kawaida kwa wanasiasa. Katika tukio hilo, pia wakristo nao walifanya ibada ya kumuombea mbunge huyo.
Nape alisema aliamua kuwakutanisha pamoja waumini wa dini hizo ili kuonyesha umoja na mshikamano miongoni mwa wapiga kura wake.
Kabla ya tukio hilo la aina yake lilijiri Jumapili iliyopita, Jumamosi yake, katika Kijiji cha Kiwalala, wasanii walioambatana na kiongozi huyo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere,’ Mike Sangu, Chopa Mchopanga, Blandina Chagula ‘Johari’, Mark Reagan na wengineo, walipanda jukwaani kuonesha kumuunga mkono kiongozi huyo kijana mwenye historia ya upambanaji ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Steve akiwa jukwaani aliwapandisha wasanii wenzake ambao baada ya kuwasalimia wananchi, walimuelezea mbunge huyo kuwa mtu muhimu katika chama na serikali.
Wasanii hao walielezea jinsi Nape alivyohangaika kwa hali na mali usiku na mchana ili kuhakikisha CCM inabaki madarakani na kusema wakati huo wengine wanaotamba sasa walikuwa hawajulikani walipo.
Wakati wasanii hao wakisema hayo umati uliofurika kwenye mkutano huo ulilipuka kwa mayowe ya furaha na kuchagiza;
“Ndiyooo… ndiyooo…. Kweli kabisaaa”.
Mapokezi makubwa aliyopata mbunge huyo, alijikuta akitoa machozi ya kutoamini alichokiona, hasa baada ya kinamama wa kijiji cha Kiwalala kulala chini na kumruhusu kutembea kwa kuwakanyaga migongoni
Post A Comment: