Tume ya Uchumi na Makosa ya Kifedha (EFCC) nchini Nigeria, jana usiku ilikamata mabilioni ya fedha za kigeni na fedha za nchi hiyo katika jumba la kifahari la mwanasiasa mmoja.
Maafisa wa tume hiyo walifika kwa kushtukiza katika jumba hilo baada ya kupewa taarifa na ‘Msamalia mwema’ na kunasa zaidi ya $38 milioni, £27,000 na N23 milioni katika jumba hilo lililoko eneo la Ikoyi jijini Lagos.
Waziri wa Habari na Utamaduni wa nchi hiyo, Alhaji Lai Mohammed alisema kuwa mtoa taarifa zilizopelekea kukamatwa kwa mabilioni hayo ya fedha atapewa asilimia tano ya kiasi kilichopatikana.
Serikali ya nchi hiyo hivi karibuni ilieleza faida za watoa taarifa (whistleblowers) na kuahidi kuwa itawalinda.
Serikali ya Nigeria imeeleza kuwa mtoa taarifa zitakazopelekea kupatikana kwa fedha kuanzia Naira bilioni 5, atapata gawio la Naira milioni 210 huku ikiweka wazi jinsi ya kukotoa magawio mengine ya mtoa taarifa kulingana na kiasi cha fedha zitakazokamatwa.
“Kwa mfano, mtoa taarifa akitoa taarifa zitakazopelekea kubainika fedha zilizofichwa kiasi cha Naira bilioni 10, atapata asilimia tano ya Naira bilioni 1 za kwanza, na asilimia nne ya Naira bilioni 4 pamoja na asilimia 2.5 ya Naira bilioni 5 zilizobaki,” Waziri Mohammed anakaririwa na mtandao wa Vanguardngr.
Serikali ya Nigeria inaendesha oparesheni ya kukamata mabilioni yaliyofichwa na watu binafsi majumbani kwa lengo la kuyatakatisha kutokana na biashara haramu na ufisadi, ambapo kabla ya tukio la jana, tume husika ilikamata mabilioni ya fedha za kigeni kwa mmoja kati ya wamiliki maarufu wa maduka ya kubadilishia fedha jijini Lagos.
Post A Comment: