NI mtikisiko bungeni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wa upinzani wakiungana kuonesha hisia zao juu ya vitendo vya utekaji watu nchini.
Baadhi ya wabunge wametaka iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza vitendo hivyo, huku wengine wakimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kutoa tamko la faraja kwa wananchi.
Hatua hiyo imeibua mjadala mzito bungeni wakati wabunge wakichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo baadhi waliibua hoja ya vitisho walivyopewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakati yakiibuka hayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe, alitupiwa kombora kutokana na hatua yake kwenda kwenye mkutano wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki ambaye alizungumza na waandishi wa habari juzi kuhusu tukio la kutekwa kwake na watu wasiojulikana.
Wakati wabunge hao wakiibua hoja hizo zilizosababisha mnyukano, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene, walikuwa wakisimama na kukiomba kiti kiwatake wabunge hao wadhibitishe kama kuna kikundi cha utekaji ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kinachohusika na vitendo hivyo.
Mtifuano huo ulianza kuonekana baada ya kipindi cha maswali na mjibu, ambapo aliyekuwa wa kwanza kuomba mwongozo alikuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), akitaka matukio hayo kujadiliwa na Bunge kwa maelezo kwamba ni suala nyeti.
“Sisi wabunge ni wawakilishi wa wananchi na katika kipindi hiki wabunge tuko katika taharuki kubwa ya watu kutekwa na watu ambao hawajapewa mamlaka hayo na kwa siku mbili hizi wabunge wameomba kujadili suala hili lakini mwenyekiti mwongozo huo haijatolewa.
“Naibu Spika ana walinzi, Watanzania wengi huko mitaani hawana walinzi, chombo pekee kinachoruhusiwa kukamata ni Jeshi la polisi, tumeona watu hata Wizara ya Mambo ya Ndani wanasema siyo polisi, watu waliokwenda kuteka wanasema siyo Jeshi la Polisi halafu chombo kikubwa kama Bunge hatujafanya kitu,” alisema Msigwa.
Alisema mpaka sasa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amekaa kimya na kuhoji. “Sasa hili ni Bunge gani linakaa kimya, tunafanya nini hapa?,” alihoji.
Alisema Msanii Roma Mkatoli kwa sasa kisaikolojia bado ametekwa hivyo kinachotakiwa si kupelekwa kwenye vyombo vya habari bali anahitaji msaada wa wanasaikolojia.
“Huu ni mkutano wa wananchi (Bunge) kwa nini hamtaki tujadili. Waziri wa Mambo ya Ndani yuko kimya, wabunge kimya tukiomba mwingozo mnatuzuia,” alisema Msigwa.
Baada ya maelezo hayo yaliyotokana na mwongozo wa Mchungaji Msigwa, alisimama Waziri Mhagama ambapo alisema. “Mheshimiwa Mwenyekiti ningependa tu, wewe sasa kama Mwenyekiti wa Bunge hili na kwa kuwa sasa mambo haya yameendelea kuzungumzwa humu ndani.
“Wabunge ambao wanazungumza mambo haya kama wana ushahidi, wafanye utaratibu ili tuweze kulimaliza jambo hili vizuri na kuzingatia mfumo wa taratibu na sheria, sisi wabunge wote tupate nafasi nzuri ya kupata udhibitisho wa mambo haya na hatua sitahiki ziweze kuchukuliwa kwa kufuata taratibu zilizopo.
“Tumekuwa tukilieleza jambo hili, tuchukue nafasi yetu kama wawakilishi wa wananchi kulisaidia Taifa kuleta uthibitisho mezani kwako,” alisema Mhagama.
Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alijibu kwa ufupi. “Haya mambo yanazungumzwa mno, kama alivyosema Chief Whip, kiti kinalichukua na tutalifanyia maamuzi baadaye,”.
Zitto na Saanane
Baada ya mjadala huo kuisha na wabunge kuendelea kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliibua tena hoja hiyo kwa kusema ni vyema sasa ikaundwa Kamati Teule ya kuchunguza vitendo vya utekaji.
Alisema licha ya kwamba Waziri Mhagama, kutoa maelezo juu ya suala hilo na kiti kuyakubali, lakini hayaendani na kanuni za Bunge.
“Mtanzania aliyepotea Ben Saanane ni suala ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu, si suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa.
“Si suala linalopaswa wabunge wabebe uthibitisho walete mezani kwasababu taarifa zilizopo sasa na ziko jeshi la polisi zinaonesha kwamba Novemba 15 Ben Saanane kwenye mawasiliano yake ya simu kuanzia asubuhi alikuwa maeneo ya Tabata.
“Akaenda maeneo ya Mikocheni akatumia muda mwingi sana maeneo ya Mwenge akapelekwa ama akaenda Mburahati saa nne usiku ya mwezi Novemba simu yake ikapoteza mawasiliano tangu hapo hajawahi kuwa trace (kuonekana) tena.
“ Na haya maelezo yako polisi na ukifuatilia Jeshi la Polisi wanakwambia tumefikia mwisho. lakini mwelekeo wetu unaonyesha kuwa waliomchukua Ben Saanane ni (anataja moja ya taasisi nyeti ya mambo ya usalama) na mwenyekiti wewe ume-save (umefanya kazi) katika Kamati ya Usalama na Mambo ya Nje, unafahamu sheria ya usalama wa taifa kifungu namba tano kifungu kidogo cha pili kinapiga marufuku usalama wa taifa ku-enforce laws (kusimamia sheria).
“Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata hata wakimwona mwizi hivi, sheria inakataa kwasababu ya kuepuka haya mambo ambayo tunayo na sasa hivi kumekuwa na matatizo, hatuyapatii ufumbuzi nyinyi mnafahamu.
“Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Kibanda (Absalom) alikamatwa akateswa, akaumizwa na leo jicho lake moja halioni, lakini hadi leo hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa.
“Kulingana na tukio kama hilo katika mazingira kama haya, hatuna namna na katika historia nyinyi wenyewe ni mashahidi ambao mmekaa bungeni muda mrefu, haijatokea Bunge hili kujadili usalama wa taifa kwa mara ya kwanza tunaivuka hiyo taboo (miiko).
“Watu wamechoka na naomba kwa mujibu wa kanuni 120 ya Bunge, natoa taarifa rasmi kwamba nitaleta hoja binafsi ndani ya Bunge ili Bunge liunde Kamati Teule ya kufanya uchunguzi wa matukio yote ya upoteaji matukio yote ya mauaji na matukio yote ambayo yanaweza kujenga taswira hasi dhidi ya usalama wa taifa katika nchi yetu,” alisema.
Alisema pia zipo Kamati za Bunge ambazo kuna baadhi ya masuala hazipaswi kupelekewa na Spika, bali zinapaswa kufanya zenyewe.
“Ndiyo maana Bunge lina utaratibu wa taarifa maalum, tulitarajia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ingetuletea taarifa maalumu kuhusu mambo haya badala ya kusubiri mpaka wabunge wazungumze.
“Tuanze kujianika, niliwaeleza its taboo kuongelea usalama wa taifa ndani ya Bunge, lakini leo tunaongelea kwasababu utaratibu unaoendelea,” alisema.
Simbachawane aja juu
Baada ya maelezo hayo, Zitto alikaa baada ya Waziri Simbachawene kusimama kumpa taarifa ambapo alisema, pamoja na uelewa wa Zitto juu ya mambo mbalimbali ikiwamo Kanuni za Bunge, amejadili Usalama wa Taifa ili hali akijua hairuhusiwi.
“Anazungumzia suala la Usalama wa Taifa ambalo haliruhusiwi kujadiliwa na Bunge. Lakini Zitto anautuhumu Usalama wa Taifa kwamba umeshiriki katika vitendo vya utekaji, je anaweza kulithibitishia Bunge hili, sababu anafahamu nimakosa kufanya hivyo its taboo (ni mwiko).
“Anasema imebidi tuvuke mipaka na sasa anauingiza usalama wa taifa katika kuutuhumu kwa jambo ambalo sina uhakika kama anaushahidi wa kutosha, kwahiyo nimwombe tu zitto alete ushahidi wa kulithibitishia Bunge hili kwamba usalama wa taifa ndio waliomshikilia Ben Saanane.
Bashe
Kabla Zitto hajasimama kupokea taarifa hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliomba kumpa taarifa Simbachwene ambapo alisema “Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri Simbachawene.
“Kwamba mimi Hussein Mohamed Bashe, nilikamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, acheni unafiki, acheni unafiki, we are all Tanzanians (wote ni Watanzania) hamjawahi kunyanyaswa ninyi, acheni mimi ni mwana CCM, I don’t care (sijali).
“Mimi nimekamatwa na usalama, nimeonewa in this country acheni unafiki, tunavumilia mambo mengi, acheni, hamjawahi kuwa humiliated,” alisema Bashe kabla ya kukatishwa na Mwenyekiti Zungu.
Baada ya Bashe kukaa, Zungu alisema kiti kilishalichukua jambo hilo na kuahidi kulipeleka mbele likajadiliwe kwa kina.
Aliporuhusiwa kuendelea na mchango wake, Zitto alisema. “Mwenyekiti mimi nimetoa taarifa kwa mujibu wa kanuni ya 120 ya kuunda kamati teule na ndio taarifa inatakiwa kufanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni.
“Nataka nimkumbushe George (Simbachawene), ni rafiki yangu, ni ndugu yangu kabisa, waliokwenda kuvamia Clouds Media ni kikosi cha ulinzi cha Rais na ninaweza kuthibitisha, aliyekwenda kumtolea bastola Mbunge wa Mtama (Nape Nnauye) ni Afisa Usalama na ninaweza kuthibitisha kama Bunge linaweza likaunda chombo cha kukataa nikathibitishe hayo niko tayari kuthibitisha,” alisema Zitto.
Aeshi na vitisho
Kwa upande wake Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM), akichangia hotuba hiyo ya Waziri Mkuu, pamoja na mambo mengine alisema. “Nilikuwa sitaki kusema lakini ngoja hili niseme, tena mimi sikutishwa kwa maneno, yeye mwenyewe nilikutana naye uso kwa uso akiniambia, ‘nyie wabunge mmezidi unafiki’ kwa bahati mbaya zaidi maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni (Ally Hapi), akasema ‘Wabunge mmezidi unafiki, na nita-deal na nyie nikianza na wewe’.
“Mimi leo Mheshimiwa, Dar es Salaam sikanyagi, na ninaiogopa, yaani nilikuwa nimei-miss mno, baada ya kutishwa nimeogopa inabidi nikae Dodoma na Sumbawanga, kwa hiyo nilitaka tu nisema kwamba naliarifu Bunge na familia yangu ijue kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam miongoni mwa watu aliowatisha ni pamoja na mimi.
“Mengine mabaya siyasemi, wala mazuri yake siyasemi, nasemea hili kwa usalama wa nafsi yangu, najua yapo mazuri aliyoyafanya, yapo mabaya aliyoyafanya, lakini mimi naomba niseme hilo moja tu kwamba, ni bora tukaliangalia kwa makini niko tayari kuhojiwa, nipo tayari kuja kusema, na nikatoe ushahidi kwa sababu nilikuwa hoteli inayoitwa Colosseum niliitwa mbele ya Mkuu wa Wilaya na akanitisha,” alisema Aeshi.
Ridhiwani
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema hivi sasa kumekuwa na malalamiko mengi mbayo yanahitaji majawabu kama siyo majibu ya haraka ili kuondoa sintofahamu walizonazo wananchi.
“Hakuna sababu ya Mwigulu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanaishi kwa wasiwasi juu…nikuombe sana, hakuna sababu ya mtu kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanalalamika juu ya hali ya kiusalama katika maisha yao, mimi binafsi niishauri serikali yangu, unapojibu jambo lolote lile unatoa wananchi wasiwasi na wanapata amani,” alisema.
Nkamia
Naye Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alimshangaa Dk. Mwakyembe kuonekana kwenye mkutano wa Roma akisema, wakati mwingine viongozi wa serikali wanamchonganisha Rais na wananchi bila sababu.
“Serikali lazima iwe active (imara) lakini siyo kuwa active kwa kukosea, nitie mfano samahani sana, jana (juzi) nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari, wa yule bwana anaitwa Roma Mkatoliki, hivi Waziri wa Habari alienda kufanya nini pale?
“Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia lakini ni afadhali uambiwe ukweli, Waziri wa Habari alikwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatoliki, anampisha na kiti, anayeongoza mkutano ule Zamaradi Kawawa ambaye ni Ofisa wa Serikali.
“Hivi kesho mtu akikwambia wewe ndiye ulimteka Roma utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini you take it, at the end of day (unauchukua na mwisho wa siku) unaweza ukafanya marekebisho.
“Ebu liangalieni hili ilitokea wapi mpaka waziri akakosa kiti, alafu huyu mtu binafsi anafanya Press Conference wewe unaenda kufanya nini? What are doing there, alafu leo kina Nkamia wakisema ukweli huku kuna watu wanasema, unajua ni kwa sababu alikosa uwaziri, this is principle, we have to tell you the truth (lazima tuwaambie ukweli),” alisema.
Post A Comment: