BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaachia kati ya Sh. bilioni 400 na 500 kwenye benki mbalimbali nchini kuanzia Alhamisi ijayo ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo.
Aidha, BOT imezitahadharisha benki hizo kuwa makini na utoaji wa mikopo ili iwe yenye tija ambayo itawezesha kubadili maisha ya Watanzania na kurudi kama inavyotakiwa.
Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu, aliyasema hayo jana baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa ripoti ya tisa ya hali ya uchumi wa Tanzania, iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB).
Ripoti hiyo ina kichwa cha habari cha 'Fedha Iliyo Karibu', ikiwa na mada mahsusi ya upatikanaji wa huduma za fedha kwa wote.
“Tunahakikisha benki zinapata fedha za kutosha na kuziba mapengo, ila tunawataka kukopesha kwa umakini mkubwa," alisema Gavana Ndulu na kuongeza kuwa:
"Tutawapa asilimia mbili kati ya 10 (ya fedha) tunazoshikilia kwa benki ambazo tunafanya nazo kazi.”
Alisema katika utekelezaji wa hilo, taratibu za kisheria lazima zifuatwe ikiwamo kutoa notisi kwa siku 21 kwa benki hizo.
Wakati BoT ikifanya hivyo, ripoti ya WB iliyotolewa jana imeeleza kuwa kuna malalamiko dhidi ya sera ya fedha ambayo imebana na kuondoa fedha hizo kwenye mzunguko na kusababisha hali ngumu kwa wananchi.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa kwa takribani mwaka mmoja mtawanyiko wa fedha umepungua kutoka asilimia 16.2 Januari mwaka jana hadi asilimia nne Januari, mwaka huu.
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa fedha za akiba zimepungua kwa asilimia moja Januari mwaka huu, kutoka kwenye ongezeko la asilimia 16.3 Januari, mwaka jana.
Akizungumza katika Jubilei ya miaka 50 ya BOT iliyofanyika katika ukumbi wa Benki hiyo, Mtaa wa Mirambo jijini Dar es salaam Juni 22, mwaka jana, Rais John Magufuli aliagiza kuanzishwa kwa akaunti moja fedha za serikali.
Uanzishwaji wa akaunti hiyo ulikuwa una lengo la kudhibiti fedha za serikali kutumika vibaya na kukopeshwa kwao yenyewe kwa riba.
Hata hivyo, wachumi mbalimbali walisema utaratibu huo pia una athari katika mzunguko wa fedha na matokeo yake kuonekana kwenye shughuli za kiuchumi.
Lakini Prof. Ndulu alipoulizwa kuhusu kuadimika kwa fedha, alisema inatokana na serikali kuziba mianya yote ya uvujaji wa fedha zake na kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo ambayo inahudumia wananchi wengi.
Kwa mujibu wa Prof. Ndulu, mageuzi yoyote yana gharama zake na kwamba itafikia mahali kila mmoja atanufaika.
Alisema pamoja na kuwapo kwa malalamiko kwa nchi kukopa zaidi, fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi kama barabara ambayo itarithishwa kizazi hadi kizazi na ambayo inachochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, alithibitisha kuwa uwekezaji wa serikali na sekta binafsi ndiyo kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini.
Ripoti ya WB imebainisha kuwa uwekezaji wa serikali ulibaki asilimia 0.5 mwaka 2006-2010 hadi 2011-2015, huku sekta binafsi ikiporomoka kutoka asilimia 2.9 hadi 2.3 kwa miaka hiyo.
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa WB kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird, alisema uchumi wa Tanzania ulionyesha ustahimilivu kati ya ukuaji unaosuasua katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara mwaka jana.
Mkurugenzi huyo alisema serikali inastahili pongezi kwa kuinua makusanyo ya mapato ya ndani hadi asilimia 14.5 ya pato ghafi, ikiwa ni matokeo ya juhudi za kupunguza misamaha ya kodi na kudhibiti rushwa.
Awali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema serikali inafanya jitihada mbalimbali kupunguza umaskini kwa kuwa kwa sasa asilimia 27 ya Watanzania wana umaskini.
Post A Comment: