SIKU chache baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kuliambia Bunge kuwa Serikali haijui kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane aliko na zaidi akipinga taarifa za kutekwa, familia ya kijana huyo imesema juhudi zao za kumtafuta zimegonga mwamba.
Akizungumza , baba mzazi wa Ben Saanane, Focus Saanane, ameiomba Serikali pamoja na vyombo vya dola kusaidia juhudi za kumtafuta, kwani juhudi zao zimegonga mwamba na suala hilo lipo nje ya uwezo wao kwa sasa.
"Toka mwanangu Ben apotee imepita miezi sita na hakuna jitihada zilizofanyika za kumtafuta, hata kama zimefanyika basi nguvu ni ndogo sana, hivyo basi, sisi kama familia tunaiomba Serikali pamoja na vyombo vya dola kusaidia juhudi za kumtafuta,” alisema.
Suala la kutoweka kwa Ben Saanane liliibuka kwa mara nyingine wiki hii kiasi cha kutikisa mhimili wa Bunge, kabla ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hajahitimisha kwa kusema kuwa Serikali inachunguza vitendo vyote vya utekaji.
Kuibuka kwa suala la Ben Saanane kulichochewa na tukio la kutekwa kwa mwanamuziki wa Bongo fleva, Roma Mkatoliki na wenzake.
Wakati Roma na wenzake wakichukuliwa mateka kwa siku tatu na kisha kuachiwa, Saanane tangu atoweke Novemba mwaka jana hadi sasa hakuna yeyote wala chombo cha dola kinachofahamu mahali alipo.
Baba huyo wa Ben ameiomba Serikali kuongeza jitihada za kumtafuta mtoto wao.
Alisema hadi sasa familia hiyo imejitahidi kufanya uchunguzi wa sababu za kupotea kwa mtoto wao, lakini jitihada hizo hazijazaa matunda na kwamba tegemeo lao kubwa limebaki kwa vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla.
“Sisi kama familia tumeshafanya jitihada mbalimbali, lakini hatujafanikiwa, kilichobaki ni kuiangalia Serikali ili itusaidie, maana hata tukiamua kutumia vyombo vya nje kumtafuta Ben bado tutapitia mikononi mwa Serikali, hivyo ni dhahiri kuwa Serikali ina nafasi kubwa ya kutusaidia kumtafuta,” alisema.
Pamoja na hilo, baba mzazi wa Ben aliliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano kuendelea kutumia vyema vikao vinavyoendelea sasa bungeni kuisisitiza na kuishauri Serikali juu ya umuhimu wa kumtafuta mtoto wao, kwani ni tegemeo kubwa kwa familia hiyo na taifa kwa ujumla.
Mapema wiki hii akijibu kauli za wabunge ambao walipiga kelele za kuitaka Serikali imtafute Saanane, huku wengine wakidai kuwapo kwa kikundi ndani ya taasisi za usalama ambacho kinatekeleza vitendo vya utekaji na utesaji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipuuza taarifa hizo.
Masaju alisema taarifa kwamba Ben Saanane ametekwa hazina ukweli, kwa sababu hakuna ushahidi wowote.
Alisema ili kuthibitisha kuwa mtu amekufa kwa mujibu wa sheria ya ushahidi lazima iwe imepita miaka mitano.
“Hatuna taarifa za Ben na haijulikani kama ametekwa au amejificha au yupo wapi. Huwezi kusema Ben Saanane ametekwa wakati huna ushahidi, inawezekana watu wasiokuwa na nia njema na Serikali hii wanafanya uhalifu kwa sababu huwezi kusema kwamba Ben Saanane amekufa.
“If you have serious information juu ya mambo ya uhalifu, pelekeni kwenye vyombo vya dola… hatuwezi kufanya hivi, sheria yetu ya ushahidi inasema ili kuthibitisha kuwa mtu amekufa miaka mitano iwe imepita, kifungu cha 100 cha sheria ya ushahidi kinaeleza hilo,” alikaririwa Masaju.
Post A Comment: