VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba leo watakuwa kwenye uwanja wa Uhuru
Dar es Salaam kucheza na Ruvu Shooting katika mechi inayotarajiwa kuwa
ya kuvuta nikuvute.
Mechi hiyo ambayo Simba ipo ugenini, inatarajiwa kuwa na mvuto wa
aina yake huku mashabiki wa soka wakitamani kuona mwenendo wa Simba kama
utaendelea au utaishia njiani kama ilivyo kawaida yake katika misimu
iliyopita kufanya vizuri na kuvurunda mwishoni.
Presha kubwa inatarajiwa kuonekana kwa wachezaji wa Simba leo, hasa
baada ya watani wao wa jadi Yanga kushinda dhidi ya Ndanda jana na hivyo
kupunguza pengo la pointi.
Simba ina pointi 41 kileleni mwa msimamo na ushindi wa jana uliifanya
Yanga kuisogelea kwa karibu ikiwa na pointi 40, hivyo ni ushindi pekee
ndio utaihakikishia Simba kutawala kwa raha kileleni mwa msimamo huo.
Baada ya mechi hizi za raundi ya 18, ligi itasimama kupisha michuano
ya kombe la Mapinduzi na itaendelea tena Januari katikati. Kocha wa
Simba, Joseph Omog alisema hana wasiwasi na timu yake kwani ameiandaa
kupambana na timu yoyote na kuibuka na ushindi.
“Simba msimu huu lengo lake ni ubingwa na ina kila sababu ya
kuuchukua, kila mechi iliyo mbele yetu ni fainali na ndivyo itakavyokuwa
kesho (leo) dhidi ya wapinzani wetu,” alisema.
Omog alisema anafahamu ugumu wa mechi zake hasa baada ya kuongoza msimamo lakini hilo halimtishi.
“Kwa vile tunaongoza sasa kila timu itataka kutufunga, lakini na sisi tumejipanga pia kuhakikisha hatuachi pointi,” alisema.
Kwa upande wa Ruvu Shooting iko nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi
ikiwa na pointi 23. Kocha wake Malale Hamsini alisema hawaiogopi Simba
bali wanaiheshimu na anaimani atapata matokeo mazuri leo.
“Simba wana timu nzuri lakini hata mimi pia timu yangu nzuri, na
hatuko kwenye nafasi mbaya sana, tunataka kushinda ili tusogee juu
kwenye msimamo kwa hiyo wenzetu wasidhani kwamba watatufuga kirahisi,”
alisema.
Mechi nyingine leo ni kati ya Azam itakayokuwa kwenye uwanja wake
Azam Complex Chamazi kumenyana na Prisons Mbeya. Azam inashika nafasi ya
nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 27 na Prisons ni ya nane ikiwa na
pointi 22.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI



Post A Comment: