Stara Sudi, mke wa
Saidi Mrisho ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, jinsi alivyoshtuka
baada ya kupokea simu aliyopiga mumewe kuwa amevamiwa na kuchomwa visu
machoni, mgongoni na tumboni.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa
Salum Njwete (34) maarufu ‘Scropion’, Stara alimueleza Hakimu Mkazi,
Flora Haule kuwa Septemba 6, saa tano usiku akiwa amelala alipokea simu
yenye sauti ya mumewe ikieleza kuwa amevamiwa.
“Aliniambia
mama Nancy nimechomwa visu hata kuona sioni hapa nilipo nipo Buguruni,”
alidai Stara ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka.
Alidai
tangu wafunge ndoa na mumewe Oktoba 2015 , Said alikuwa akifanya kazi
ya kinyozi katika saluni ya Rodgers iliyopo Tabata Sanene.
“Baada
ya kuongea na mume wangu, simu ilikatika lakini wakati natafuta nguo
nivae simu ileile ilipiga na nilipopokea sauti ya mtu mwingine iliongea
ambaye ndiye mwenye simu na aliniambia kuwa mume wangu ana hali mbaya
hivyo nifanye haraka niende Hospitali ya Amana,” alidai Stara.
Baada
ya kupata taarifa hizo, alidai alimweleza mtoto wao mkubwa, Abdul Said
(12) kuwa anaelekea Amana. Lakini kabla ya kwenda huko alichukua
pikipiki na kwenda Mabibo Hosteli anakoishi mama mkwe wake kumweleza
taarifa hiyo na kwamba waliambatana hadi Amana. Alidai wakiwa njiani,
walimjulisha mdogo wa Saidi, Yahaya Kisukari (23) kuwa kaka yako amepata
matatizo ya kuvamiwa na mtu akachomwa visu na yupo Hospitali ya Amana.
“Tulipofika
Amana, tuliruhusiwa kuingia wodini na kumuona mume wangu akiwa
amefungwa bandeji machoni na sehemu nyingine za mwili, huku damu ikivuja
sehemu mbalimbali za mwili. Hata nguo aliyovaa ilikuwa imejaa damu,”
aliiambia Mahakama na kuongeza:
“Baada
ya kumvua nguo zilizokuwa zimetapakaa damu, tulipewa rufaa kwenda
Muhimbili kwa ajili ya matibabu na wakati huo ilikuwa imeshafika saa
sita usiku.”
Stara
alidai baada ya kumuona mumewe aliyechomwa visu na mtu aliyemtaja kwa
jina la Scorpion, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni.
“Baada
ya kutoa maelezo Polisi Buguruni na askari kwenda kuchukua maelezo ya
mume wangu Muhimbili, tulikwenda kumkamata mshtakiwa Salum Njwete,”
alidai.
Alidai:
“Septemba 8, tulirudi tena Muhimbili na kupewa taarifa na daktari wa
macho aliyemfanyia upasuaji Said kuwa macho yake hayataona tena.”
Stara alidai tangu waoane na mumewe, hajawahi kupata malalamiko yoyote kuwa mwenza wake huyo ni mwizi.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI


Post A Comment: