MKULIMA aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea
shingoni, Augustino Mtitu (35), amepata pigo lingine baada ya familia
yake ya mke na watoto watano, kutoweka nyumbani na kwenda
kusikojulikana.
Familia hiyo iliyokuwa ikiishi katika Kitongoji cha Upangwani Kijiji
cha Dodoma Isanga Kata ya Masanze Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro,
imetoweka katika makazi yake hayo ikihofia vitisho dhidi yao
vinavyodaiwa kutolewa na baadhi ya wafugaji nyakati za usiku.
MTITU AIANGUKIA SERIKALI
Aidha, majeruhi huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu baada ya kupataa taarifa za familia yake kuyakimbia makazi yake, ameiangukia serikali akiiomba ichukue hatua za makusudi kuhakikisha amani inapatikana katika eneo hilo.
Pamoja na familia hiyo kuondoka katika makazi yake, pia familia
nyingine tisa zenye idadi ya watu kati ya watano na sita katika
kitongoji hicho, nazo zimeyakimbia makazi yake na kwenda kutafuta
hifadhi katika vijiji vya jirani kwa hofu kama hiyo.
Nipashe lilifika katika Kitongoji cha Upangwani kwenye nyumba
anayoishi majeruhi Mtitu na kukuta si mkewe Maria Msanga wala watoto
wake, Pili (16), Lavuma (14), Josephine (10), Misio (7) na Simon (3),
hawapo katika makazi hayo huku nyumba yao ikiwa imetiwa kufuli.
Akizungumzia na Nipashe,baba mdogo wa mke wa Mtitu anayeishi katika
kitongoji hicho pia Mwalongo Sangu, alisema familia hiyo iliondoka na
kutelekeza nyumba hiyo tangu Desemba 26, mwaka huu ikidai inakwenda
kutafuta sehemu nyingine ya kujihifadhi kutokana na tishio la wafugaji.
Sangu alisema familia hiyo ilipata hofu kutokana na maneno ya baadhi
ya wafugaji waliokuwa wanapita katika kitongoji hicho usiku wakiwa na
tochi na kuwatishia kuwa endapo wataendelea kufukuza mifugo yao katika
mashamba ya wakulima, watawafanyia vitendo hivyo wengine.
"Mimi huyo Mtitu aliyechomwa Mkuki mdomoni, ni kama mwanangu pia kwa
kuwa mkewe ni mtoto wa kaka yangu kabisa. Waliondoka na kukimbia
nyumba, hii ni siku ya pili baada ya tukio akiwa mama na watoto wake
watano na hatujui wamekwenda kutafuta hifadhi wapi. Taarifa nilionayo
wamekuwa wakitishiwa na wafugaji wanaopita usiku katika kitongiji
chetu," alisema Sangu.
Kwa mujibu wa Sangu, watoto watatu kati ya watano wa Mtitu (Lavumo,
Josephine na Misio), wanasoma katika Shule ya Msingi Nyari iliyopo
kijiji cha jirani.
Sangu alieleza kuwa hafahamu kama watoto hao watarudi kuendelea na
masomo yao kwa kuwa muda wa kufunguliwa shule hizo, umekaribia baada ya
likizo ya mwaka kumalizika.
Aliongeza kuwa familia hiyo, iliondoka katika nyumba hiyo na kuacha
kila kitu ikiwamo baadhi ya mifugo yao ya kuku na kwa sasa yeye ndiye
anayeangalia usalama wa nyumba hiyo kwa kupitia pitia akishirikina na
majirani wa kitongoji hicho.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho ambaye alijeruhiwa kichwani na sime
katika tukio hilo, Mathayo Luoga, alithibitisha familia ya Mtitu
kuyakimbia makazi yao kutokana na vitisho vya baadhi ya wafugaji
wanaopita nyakati za usiku wakiwa na tochi na kumulika nyumba hadi
nyumba.
"Mimi nimetoka hospitali Desemba 27, mwaka huu nimefika hapa na
kupewa taarifa na wananchi kuwa familia ya Mtitu imeondoka na kuelekea
kusikojulikana ikihofia maisha yao kutokana na vitisho vya baadhi ya
wafugaji wanaopita katika kitongoji chetu nyakati za usiku. Suala hili
nimelifikisha kwa Mwenyekiti wa Kijiji hiki cha Dodoma Isanga,” alisema.
Alisema kuwa pamoja na familia hiyo kuondoka, lakini zipo familia
nyingine katika kitongoji hicho ambazo pia zimeamua kuondoka na kwenda
kutafuta hifadhi katika vijiji vya jirani kikiwamo Kijiji cha Nyari
kilichopo Kata ya Zombo Tarafa ya Ulaya.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Alexona Joakim, alisema mke wa
Mtitu alimuaga kuwa anaondoka na watoto wake kutokana na tishio la
baadhi ya wafugaji kupita nyakati za usiku na kutishia usalama wao.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI



Post A Comment: