![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa
ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa
kujiunga na vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli
kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti
vyenye sifa.
Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni
wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na
kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo
jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea
mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada
kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato
cha sita.
Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha
wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya
kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia
wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu
anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki
utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu
Waziri.
Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo
zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa
watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika
hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha
sita waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa
pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu
wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya
Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya
Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei
mtu sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha
sita, kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa
nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,”
alieleza Waziri Ndalichako.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: