![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), Luhaga Mpina amesema mawaziri walioteuliwa na Rais John
Magufuli si waoga na wanatekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na
kumshauri Rais katika masuala mbalimbali.
Mpina aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika
kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu mkoani Simiyu huku akisikitika kuwa
maneno yanayotolewa dhidi ya mawaziri na manaibu na viongozi wa vyama
vya upinzani kuwa wao ni waoga na hawamshauri Rais si sahihi.
Alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakibeza utendaji wa Baraza la Mawaziri na kuwaita waoga wasiomshauri Rais.
“Wapo wale wenzetu wa upande wa pili ambao ni wapinzani wamekuwa
wakitubeza mawaziri tulioteuliwa na Rais Magufuli kuwa tumekuwa waoga na
hivyo kushindwa kumshauri na kulifanya taifa kusinyaa, hii si kweli.
Nyinyi ni mashahidi, mmeona jinsi tunavyochapa kazi,” alisema.
Katika kudhihirisha kuwa wanatekeleza wajibu na kumshauri Rais, Mpina
alisema Serikali iliamua kumnyang’anya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye shamba la hekta 33 kwa kushindwa kuliendeleza.
“Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya
kumiliki ardhi ya shamba namba 3074 lililopo Mabwepande, Dar es Salaam
lililokuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika
hati ni Frankline Sumaye huu ni ushauri Rais alipewa na Waziri wa Ardhi
na akachukua hatua,” alieleza Mpina.
Alisema wataendelea kuchukua hatua bila ubaguzi wa aina yoyote kwa
wasiotaka kufanya kazi kwa kufuata utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Post A Comment: