![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
IKIWA ni zaidi ya siku 10 zimepita tangu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu (HESLB), kutangaza hadharani majina 142,000 ya wadaiwa
sugu wa mikopo ya elimu ya juu wanaodaiwa Sh bilioni 239, wadeni hao
wamejitokeza na kuanza kulipa.
Akizungumza hili mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam,
Ofisa Mwandamizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Veneranda
Malima, alisema tangu watoe tangazo la wadaiwa hao, kila siku hupokea
wadaiwa 300 wanaokwenda kuchukua taarifa za madeni yao na wameanza
kulipa.
“Ni kweli kabla ya kutoa majina ya wadaiwa hao, Novemba 4, mwaka huu
pia tulitangaza kuwa tutachapisha majina ya wadaiwa hao ifikapo Novemba
14, mwaka huu na baada ya tangazo kutoka tulianza kupokea wadaiwa wengi
waliokuja kuangalia taarifa za madeni yao na wameshaanza kulipa”,
alisema Malima.
Akizungumzia kiasi cha malipo kilicholipwa ndani ya muda huu tangu
kutangazwa kwa tangazo hilo, Malima alisema taarifa rasmi ya kiasi cha
fedha kilichokusanywa kwa takribani siku 10 hadi 13, tangu watoe tangazo
hilo, kitatolewa baada ya wahasibu kupitia hesabu kuona kiasi cha fedha
kilicholipwa benki.
“Kuhusu idadi ya fedha tutatoa taarifa baadaye kidogo, kwa sababu
hivi sasa wadaiwa wanaendelea kulipa madeni yao kupitia akaunti ya bodi
ya benki, na wahasibu wetu watapitia kuona hadi sasa kwa kipindi cha
wiki moja ni kiasi gani kimelipwa”, alisema Malima.
Akizungumzia madeni ya wadaiwa hao, Malima alisema yapo tofauti
kulingana na aina ya kozi, muda na kiwango cha mkopo alichopewa na
kuwataka wale ambao bado hawajaitikia mwito huo, kuhakikisha
wanafuatilia madeni yao na kuyalipa.
“Tulichopanga ni baada ya ule muda wa siku 30 kumalizika, ambao
unaisha Desemba 13, hatua zaidi tutazichukua na hatua zenyewe
zinajulikana kama sheria ya mikopo hiyo inavyoeleza,” alisisitiza
Malima.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: