![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ameshtukia safu ya benchi la ufundi
la mahasimu wao, Yanga ikiwepo kuanza mapema maandalizi yao kwa ajili
ya mzunguko wa pili na kuwataka wachezaji wake wote kufika kwa wakati
siku ambayo wamepanga kuanza mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Juzi Ijumaa Yanga, ilitangaza benchi jipya la Ufundi ambalo litakuwa
chini ya kocha Mzambia George Lwandamina huku aliyekuwa kocha mkuu wa
timu hiyo, Mholanzi Hans Pluijm akipandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa
Ufundi wa klabu hiyo.
Akizungumza hivi karibuni Omog, alikiri kuwa mikakati ya wapinzani
wao Yanga imemtia hofu na kutoa mwito kwa wachezaji wake popote walipo
kufika kwa wakati ili kuanza maandalizi yao ya mzunguko wa pili wakiwa
wote na kupeana mbinu mbadala, ambazo zitaweza kuwasaidia kuwapa ubingwa
msimu huu.
“Lazima nikiri kuwa Yanga ndiyo timu ambayo inanipa presha kwa sababu
tunatofautiana nao kwa pointi mbili, lakini kitendo cha kubadilisha
benchi lao la ufundi nacho kinaonesha namna walivyokuwa makini katika
kuendelea kuwa tena mabingwa msimu huu kutokana na ubora wa kocha na
Mkurugenzi wa ufundi,” alisema Omog.
Kocha huyo alisema ingawa hafahamiani vizuri na Lwandamina, lakini
anaonesha ni kocha mwenye uwezo mkubwa, kutokana na mafanikio aliyoipa
Zesco United, sawa na Pluijm ambaye amepewa cheo cha Ukurugenzi hivyo
anaamini Yanga ya mzunguko wa pili itawasumbua zaidi kutokana na uwepo
wao.
Alisema anataka kuanza maandalizi mapema, lengo likiwa ni kurudisha
umoja na ufiti wa wachezaji wake pamoja na kuwajenga kisaikolojia kwa
sababu watakuwa wakicheza kwa presha kutokana na tofauti ya pointi mbili
kati yao na mahasimu wao Yanga.
“Tutacheza kwa presha kubwa kwa sababu ya tofauti ya pointi mbili
hofu yetu ni kuhofia kupoteza mchezo kwamba wapinzani wetu watatupita na
kibaya zaidi tuna mechi nyingi za ugenini mzunguko wa pili", alisema na
kuongeza:
“Endapo tutaanza maandalizi kwa pamoja niwazi tutaweza kurudisha ari
ya waliyokuwa nayo wachezaji wetu na kuweza kupambana na Yanga kwenye
mbio za ubingwa,” alisema Omog.
Simba imepoteza michezo miwili sawa na Yanga kwenye mzunguko wa
kwanza na tofauti yao ni pointi mbili na kocha Omog, amepania timu hiyo
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu na ndiyo maana amewasisitiza
wachezaji wake kujitokeza kwa wingi siku ya kwanza ya mazoezi ya timu
hiyo.
Wakati huo huo, Omog amewataka viongozi wa klabu hiyo kusajili wachezaji watatu tu, ambao ni kipa, beki na mshambuliaji.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: