SIKU moja baada ya viongozi mbalimbali akiwemo Rais mstaafu wa Awamu
ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuonya nchi kupoteza mwelekeo miaka 17 baada
ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imeelezwa kuwa Rais
wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli ameanza kurejesha misingi
hiyo.
Mwinyi na viongozi wengine akiwemo pia Waziri Mkuu mstaafu, Jaji
Joseph Warioba wakizungumza kwenye midahalo ya Kumbukumbu ya kifo cha
Mwalimu Nyerere juzi, walieleza shaka juu ya nchi kuanza kumeguka katika
misingi ya ukabila na udini, hatua waliyosema inatishia umoja na
mshikamano wa kitaifa.
Akizungumzia hofu hiyo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya
Maadili, Amani na Haki za Jamii kwa Madhehebu ya Dini nchini, Askofu
William Mwamalanga alisema Rais John Magufuli ameanza kuirejesha nchi
katika misingi yake.
“Ni vizuri kueleza hofu iliyopo lakini ni vizuri zaidi kutambua
jitihada zinazochukuliwa na Rais wa sasa Magufuli katika kurejesha nchi
katika misingi ya Azimio la Arusha ambayo iliweka misingi ya uongozi.
“Hili lipo wazi, Mwalimu alikemea rushwa na watu waliogopa rushwa sawa
na sasa ambapo hofu ya rushwa ipo tofauti na ilivyokuwa hapo katikati.
Rais Magufuli amechukua hatua nyingi kama kuhimiza uwajibikaji na
kukemea matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu,”
alisema Askofu Mwamalanga.
Alisema mbali ya kurejesha misingi ya uongozi, Rais Magufuli pia
ameweza katika kipindi cha muda mfupi kujenga heshima ya nchi ya
Tanzania nje, kutokana na na jitihada zake za kutetea wanyonge,
kuheshimu utu wa mtu, kuhamasisha umoja na mshikamano, kukemea rushwa,
kulinda maliasili za nchi, kuhamasisha nchi na Mataifa ya Afrika
kujitegemea na kukataa misaada yenye masharti yasiyo na staha kwa Taifa
kama alivyofanya Mwalimu Nyerere.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: