Meneja wa majogoo wa jiji (Liverpool), Jurgen Klopp amekosoa mpango
wa baadhi ya klabu za soka nchini England pamoja na nchi nyingine za
barani Ulaya wa kufanya usajili kwa kutumia pesa nyingi kwa mchezo
mmoja.
Klopp amepinga mpango huo kwa kusema hawezi kufanya kitu kama hicho
katika falsafa zake za soka anazozitumia kila napokua ofisini, na badala
yake amejipanga kufanya jambo tofauti katika harakati za usajili akiwa
na klabu ya Liverpool.
Klopp amekosoa mpango huo, huku mahasimu wake Man Utd wakiwa katika
mchakato wa kutaka kukamilisha dili la usajili wa kiungo kutoka nchini
Ufaransa na klabu bingwa nchini Italia Juventus FC, Paul Pogba ambalo
litawagharimu kiasi cha Pauni milioni 100.
Akifanyia mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha ESPN
kilichopo nchini Marekani, meneja huyo kutoka nchini Ujerumani, alisema
huenda ikawa hasara kubwa kwa klabu inayotumia mfumo wa kutumia pesa
nyingi kwa mchezaji mmoja, pale inapotokea anaumia ama anacheza chini ya
kiwango na ilivyotarajiwa.
“Kama unamsajili mchezaji kwa ada ya Pauni milioni 100, na ikitokea
anapata majeraha, ama anacheza chini ya kiwango hiyo inakua ni hasara
kubwa kwa klabu,” Alisema Klopp.
“Mchezo wa soka unatakiwa kubadilika siku hadi siku kutokana na
mazingira yaliopo, hivyo unapaswa kuwa muangalifu na mbunifu katika
matumizi ya pesa za usajili wa wachezaji, kwani jambo hilo ndio linatoa
mustakabali mzima wa msimu wako wa ligi.
Alisema anajitahidi kutumia pesa katika mfumo mzuri kwa kuwasajili
wachezaji wenye thamani ya kawaida ili aweze kuipa faida klabu ya
Liverpool na ndio maana ameona umuhimu wa kuwa na mshambuliaji kutoka
nchini Senegal, Sadio Mane ambaye alimsajili akitokea Southampton, kwa
ada ya Pauni milion 34 pamoja na Georginio Wijnaldum aliyetokea
Newcastle United kwa kiasi cha Pauni milion 23, sambamba na Joel Matip
na Loris Karius.
Klopp sambamba na kikosi chake kwa sasa wapo nchini Marekani
wakijiandaa na msimu mpya wa ligi ya nchini England kwa kushiriki
michuano ya International Champions Cup (ICC), na mchezo ujao watacheza
dhidi ya AC Milan katika uwanja wa Levi uliopo katika kitongoji cha
Santa Clara jimbo la California.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: