ads

MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Jeshi la Polisi la Wanamaji, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP), Evance Mwijage (56), amedai mahakamani alipokea barua ya kufanya uchunguzi wa malalamiko ya Dk. William Morris dhidi ya Mchungaji Joseph Mwingira kumbaka na kumzalisha mke wake Dk. Phillis Nyimbi.


Kamishna Mwijage ambaye alikua Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Pwani (RCO) wakati wa tukio, alipitia maelezo ya Dk. Nyimbi (mlalamikiwa wa pili) kwamba mchungaji Mwingira alimwita kumfanyia maombi katika hoteli ya Millenium Tower, jijini Dar es Salaam lakini baadaye alifanya naye tendo la ndoa katika eneo hilo zaidi ya mara tatu na kushika ujauzito na kumzalisha mtoto.

Shahidi huyo alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gofrey Mhini anayesikiliza kesi hiyo ya madai iliyofunguliwa na Dk. Moris dhidi walalamikiwa wawili, Mchungaji Mwingira na Dk. Nyimbi ya fidia ya Sh. bilioni 7.5 kwa kuzini na kumzalisha mke wake wa ndoa.

Shahidi huyo alidai kuwa kati ya mwaka 2010 na 2012 alikuwa RCO Pwani na kwamba alipokea barua ya Dk. Moris kutoka Ofisi ya Rais ikimtaka kufanya uchunguzi wa malalamiko kuhusu Nabii Mwingira kumdhalilisha kwa kumbaka mke wake na watu wengine.

"Tulianza kuchunguza mara moja ili kujua kama ni kesi ya jinai ama ya madai, tulimwita mke wa mlalamikaji (am baye) alikuja na kutoa maelezo yake kwamba walikutana na mume wake nchini Urusi alipokwenda kusomea udaktari... baadaye walioana," alidai na kusema zaidi:

"Walipoona mlalamikaji alirejea Marekani kwa kuwa ni raia wa huko, lakini mlalamikiwa wa pili alitafuta vibali vya kumfuata mume wake; alikosa ndipo akashauriwa kwenda kuombewa kwa Mchungaji Mwingira," alidai shahidi.

Akifafanua zaidi, alidai kuwa mlalamikiwa wa pili alipokwenda kwa Mchungaji huyo alimweleza shida yake ni kumwombea mume wake arudi nchini na kwamba walibadilishana namba za simu.

"Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Nyimbi, siku moja mchungaji alimpigia simu kwamba wakutane hotelini na alipomfahamisha kwamba hapafahamu alimtaka kuchukua teksi... alipofika alijitambulisha mapokezi akaelekezwa chumba alichopanga mwenyeji wake," alidai.

"Alipofika chumbani walijadili kuhusu kumwombea mume wake kuja nchini lakini baadaye walitenda tendo la ndoa."Waliendelea kukutana kwenye chumba hicho mara kwa mara mwisho wake mlalamikiwa alishika ujauzito.

"Alipojifungua alimjulisha, mchungaji alikwenda kumwangalia mtoto na alimpa jina la Mfalme Daudi pamoja na fedha za matunzo Sh. 500,000 na kumtaka kuendelea na maisha yake kwa sababu hawezi kumwoa, ana mke wake, mawasiliano yaliishia hapo."

Kesi hiyo inaendelea Ijumaa kwa ajili ya utetezi wa Mchungaji Mwingira na Dk. Nyimbi.

Katika kesi ya msingi, Dk. Morris pamoja na mambo mengine anaiomba mahakama hiyo imwamuru Mchungaji Mwingira amlipe sh. bilioni 7.5 kama fidia ya kuzini na kuwa na uhusiano na mkewe Dk. Phillis.

Dk. Morris anadai kitendo cha mkewe kuwa na uhusiano na Mwingira, ni kwenda kinyume na ndoa yao halali na kimeharibu mipango yake ya mbele kiasi cha kumfanya apoteze matumaini ya kuishi.

Credit - Nipashe
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: